Mwakinyo ni noma kabisa aisee

Muktasari:

Kwa mujibu wa viwango hivyo, Mwakinyo kwa sasa ana jumla ya pointi 156.5 na kuwazidi mabondia kadhaa maarufu duniani.

BONDIA nyota wa uzito wa welter, Hassan Mwakinyo amepanda nafasi nne za mabondia bora duniani katika orodha ya viwango iliyotolewa na mtandao maarufu wa ngumi za kulipwa boxrec.

Mwakinyo ambaye alikuwa nafasi ya 22 kati ya mabondia 1,515, amepanda mpaka nafasi ya 18 katika orodha iliyotolewa jana na mtandao huo.

Bondia huyo anayedhaminiwa na kampuni ya michezo ya kubahatisha ya SportPesa Tanzania pia anashika namba moja katika bara la Afrika na katika viwango vya Tanzania pia.

Akizungumzia mafanikio hayo, Mwakinyo alisema kuwa juhudi zinalipa na ushindi wa TKO katika raundi ya tano dhidi ya bondia wa Argentina, Sergio Eduardo Gonzalez umempandisha chati hiyo.

“Malengo yangu yapo pale pale, kuwania ubingwa wa vyama vikubwa, hakuna haja ya kuwa na haraka, nawapongeza wadhamini wangu, SportPesa Tanzania kuwa kunipa sapoti kubwa katika mchezo wa ngumi,” alisema Mwakinyo.

Kwa mujibu wa viwango hivyo, Mwakinyo kwa sasa ana jumla ya pointi 156.5 na kuwazidi mabondia kadhaa maarufu duniani.

Bondia wa Zimbabwe, Charles Manyuchi ndiye anamfutia Mwakinyo kwa kushika nafasi ya 41 katika viwango hivyo. Manyuchi amekusanya pointi 76.03. Bondia huyo ameshuka nafasi tano ambapo awali alikuwa wa 36 kwa kupata pointi 114.5.

Bondia wa Ghana, Patrick Allotey amekuwa wa tatu katika bara la Afrika kwa kushika nafasi ya 130 kwa kupata pointi 16.72 huku Ali Funeka wa Afrika Kusini ambaye awali alikuwa wa 88 kwa pointi 63.08 ameshuka mpaka nafasi ya 148 kwa kupata pointi 13.85.

Bondia wa DR Congo anayeishi Afrika Kusini ameshuka mpaka nafasi ya 133 kwa kupata pointi 16.32. Awali, bondia huyo alikuwa wa 31 kwa kupata pointi 126.

Mmarekani, Jurreth Hurd aliyekuwa anaongoza kwa kuwa na pointi 602.7 ameshuka mpaka nafasi ya nne duniani.