Mwakinyo aletewa zaidi ya Tinampay

Friday October 16 2020
mwikanyo pic

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo atakuwa na kibarua cha kutetea ubingwa wake wa Dunia wa WBF na kuwania mkanda mwingine wa mabara wa IBA, dhidi ya Jose Carlos Paz raia wa Argentina, Novemba 13 kwenye Ukumbi wa Next Door Arena, Masaki, Dar es Salaam.

Pambano hilo huenda likawa na upinzani maradufu kwa Mwakinyo kulinganisha na lile la Novemba mwaka jana alipozichapa na Mfilipino, Arnel Tinampay, matokeo yakawagawa mashabiki.

Pambano la Novemba 13, Mtanzania huyo atacheza na Paz bondia mwenye rekodi na kiwango bora zaidi kulinganisha na cha Tinampay, ingawa Mwakinyo amesisitiza kumaliza pambano hilo kwa matokeo yasiyokuwa na utata ya Knock Out (KO) siku hiyo.

“Najiandaa vizuri, siwezi kupigwa, itakuwa ni zaidi ya burudani siku hiyo kwa mashabiki wangu,” alisema Mwakinyo jana wakati wa kutambulisha pambano hilo.

Paz au kwa jina la utani Puro ni bondia namba saba kati ya 76 nchini kwao na wa 98 kati ya 1,997 duniani mwenye hadhi ya nyota mbili na nusu sawa na Mwakinyo ambaye ni namba moja nchini na wa 87 duniani.

Muargentina huyo mwenye rekodi ya kushinda mapambano 23 (13 kwa KO), kupigwa mara 11 (6 kwa KO) na sare moja amemzidi ubora Tinampay bondia aliyempa upinzani Mwakinyo mwaka jana ambaye ni wa 162 duniani.

Advertisement

Mkurugenzi wa kampuni ya Jackson Group, ambao ndiyo waandaaji wa pambano hilo, Kelvin Twissa alisema mbali na Mwakinyo, mabondia kutoka Kenya, Zimbabwe na DRCongo pia watazichapa siku hiyo kuwasindikiza Mwakinyo na Paz.

“Aliyekuwa bingwa wa dunia wa WBC kwa wanawake, Fatuma Zarika wa Kenya atacheza na Patience Mastara wa Zimbabwe na Zulfa Yusuph Macho wa Tanzania atacheza na Alice Mbewe wa Zimbabwe.

 

Advertisement