Mwakinyo aanza kurudi mdogo mdogo

Muktasari:

Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imesema Mwakinyo hajashuka kiwango na kilichotokea ni suala la kimtandao.

Dar es Salaam. Bondia Hassan Mwakinyo ameanza kupanda polepole kwenye viwango vya ngumi vya dunia baada ya wiki iliyopita kuporomoka kwa hadi nafasi ya 86.

Hadi jana, bondia huyo namba moja nchini alikuwa amepanda kwa nafasi saba na kuwa bondia wa 79 kwenye uzani wa super welter (kg 69) duniani.

Wiki iliyopita mtandao wa ngumi za kulipwa wa dunia ulitaja viwango vipya na Mwakinyo kuporomoka kutoka nafasi ya 24 hadi 86 kabla ya jana asubuhi kupanda kwa nafasi nne na kuwa wa 82 na baadaye mchana kufikia 79.

Taarifa iliyotolewa na boxrec ilisema kulikuwa na tatizo la kiufundi na mabondia walioshushwa viwango akiwamo Mwakinyo watakuwa wakipanda polepole.

Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa Tanzania (TPBRC) imesema Mwakinyo hajashuka kiwango na kilichotokea ni suala la kimtandao.

Hata hivyo, kwa mujibu wa Boxrec, Mwakinyo hawezi kupanda na kurudi kwenye nafasi yake ya awali kwa haraka na itamlazimu acheze na kushinda mapambano yake yajayo ili azidi kujiimarisha katika nafasi nzuri zaidi.

Bondia huyo aliyewahi kuwa namba moja Afrika, alisalia katika nafasi ya sita katika orodha ya mabondia bora wa bara hili huku Emmany Kalombo wa Afrika Kusini akiongoza akifuatiwa na Wale Omotoso wa Nigeria ambaye wiki iliyopita alikuwa namba moja.

Mwakinyo amewahi kuwa namba 16 duniani Septemba, 2018 alipomchapa aliyekuwa bondia namba nane wakati huo, Sam Eggington nchini Uingereza.

Baadaye aliwachapa kwa KO, Eduardo Gonzalez wa Argentina huko Kenya, Joseph Sinkala na Said Yazidu mjini Tanga kabla ya kushinda kwa pointi dhidi ya Mfilipino, Arnel Tinampay jijini Dar es Salaam.

Hivi karibuni, pambano lake na Jack Culcay bondia namba saba wa dunia lililokuwa limepangwa kufanyika huko Ujerumani liliahirishwa baada ya shughuli zinazojumuisha mijumuiko kusimamishwa karibu kila sehemu duniani baada ya kuibuka kwa janga la virusi vinavyosababisha ugonjwa wa corona ambavyo vimeathiri idadi kubwa ya watu.