Mwakinyo aanika mipango yake kimataifa

Wednesday June 3 2020

 

By Imani Makongoro

Baada ya kuwa kimya kwa muda mrefu kufuatia kuporomoka kwenye viwango vya ngumi duniani, Hassan Mwakinyo ameeleza mipango yake mipya.

Mwakinyo bondia namba moja nchini kwenye uzani wa super welter aliporomoka hadi nafasi ya 76 kwenye viwango vya ngumi duniani miezi kadhaa iliyopita kutoka nafasi ya 21.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu jana, Mwakinyo alisema bado ana ndoto ya kuwa bondia namba moja wa dunia.

"Nilishtuka niliposhuka, lakini nikajipa moyo kwani kama nilitoka kuwa bondia wa 179 nikafika hadi nafasi ya 16 duniani, basi hata sasa naweza nikapanda na kuwa namba moja," alisema.

Bondia huyo alisema mikakati yake ni kucheza mapambano matano mfululizo ambayo atayashinda kwa knock out (KO) kipindi hiki.

"Sitajali napigana na nani au wapi, ila nataka nicheze mapambano ambayo nitashinda kwa KO mfululizo mara tano ili rekodi yangu iwe vizuri," alisema.

Advertisement

Bondia huyo ambaye sasa ana nyota mbili na nusu kutoka nne za awali alisema promota wake, Ally Mwanzoa ameshaanza mchakato wa yeye kurudi ulingoni licha ya pambano lake lililokuwa lipigwe Ujerumani kuondoshwa kucheza.

Katika pambano hilo ambalo liliahirishwa kutokana na tahadhari ya virusi vya corona, Mwakinyo angezichapa na Jack Culcay ambaye sasa atacheza na bondia mwingine baada ya Mwakinyo kuporomoka.


Advertisement