Mwakalebela: Ushindi Yanga unaanzia kwa Gwambina

Muktasari:

Akizungumzia tetesi za wachezaji wao kutolipwa mishahara alisema suala hilo halipo na wachezaji wote wamelipwa.

Dar es Salaam.Baada ya kutoka sare nne mfululizo katika Ligi Kuu Tanzania Bara, Uongozi wa klabu ya Yanga kupitia kwa Makamu Mwenyekiti, Fredrick Mwakalebela amewatuliza mashabiki wake na kuhaidi matokeo ya ushindi yanaanza katika mchezo wao wa kesho wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Gwambina.

Mwakalebela alisema tayari wameshakaa chini na benchi la ufundi pamoja na wachezaji kuzungumza ili kupata ushindi katika mchezo huo na michezo yao ijayo.

"Tuna timu nzuri na benchi la ufundi zuri, huu ni upepo mbaya ambao umepita kwetu na tumekaa na wenzetu kuzungumza namna ya kuepukana na kikombe hiki na kuendelea kuwapa raha mashabiki na tunawaahidi waje uwanjani," alisema.

Akizungumzia tetesi za wachezaji wao kutolipwa mishahara alisema suala hilo halipo na wachezaji wote wamelipwa.

"Hatudaiwi na wachezaji na ndio maana nilisema tulikaa na wachezaji kwa sababu ya kuzungumza nao shida ipo wapi kwani kila mmoja tayari ameshatimiza wajibu wake kwa ufasaha," alisema.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro kwa kusema wachezaji wote wamelipwa mishahara na hakuna anayedai.

"Nasema hili wazi kabisa na kama mtu ajapeleka pesa nyumbani kwake basi atakuwa na matatizo, lakini huku wameshalipwa," alisema Muro.