Mwadui maji yamefika shingoni

Thursday May 16 2019

 

By Saddam Sadick

MWANZA.SARE ya mabao 3-3 waliyopata Mwadui dhidi ya Mbao FC iliitibulia zaidi timu hiyo kwenye vita ya kukwepa kushuka daraja ingawa Kocha wa kikosi hicho, Ally Bizimungu kuwatoa hofu mashabiki kwa msala huo utawapitia pembeni.

Mwadui ni msimu wake wa tano kushiriki Ligi Kuu, wamekusanya Pointi 38 na kukaa nafasi ya 19 huku wakibakiza michezo miwili kumaliza michuano hiyo.

Bizimungu alisema licha ya kwamba hali si nzuri, bado matumaini ya kubaki kwenye ligi msimu ujao yapo na kikubwa ni kushinda michezo miwili iliyobaki.

Alisema makosa waliyoyafanya mechi zilizopita ikiwamo ya Mbao ambazo hawakupata pointi tatu atahakikisha anakaa na wachezaji wake kujadili nini kifanyike ili kufikia malengo yao.

“Bado nafasi ipo ina maana tukishinda mechi mbili zilizobaki wakati huo timu zilizo juu yetu zikapoteza tunapanda juu kwahiyo hatukati tamaa,” alisema Bizimungu.

Kwa upande wake beki wa kati wa timu hiyo, Revocatus Mgunga alisema tatizo kubwa lililowagharimu hadi kufikia wakati huu kusubiri matokeo ya mwisho ni kutokuwapo muunganiko mzuri kati ya uongozi na benchi la ufundi.

“Muunganiko siyo mzuri ndani ya timu, kwahiyo kama hakuna ushirikiano lazima mambo kama haya yatokee, sisi wachezaji tutapambana kuinusuru timu kutoshuka daraja,” alisema Mgunga.

Mpaka sasa Mwadui imecheza michezo 36 na kuvuna alama 38 pekee jambo ambalo linawaumiza vichwa.

Advertisement