Mtwara chagamkieni fursa ya Umitashumta, Umiseta

Muktasari:

  • Wenyeji wa mashindano ya Umitashumta na Umiseta wametakiwa kuchagamkia fursa zitakazojitokeza wakati wa mashindano kujiunua kiuchumi.

Mtwara.Waandalizi wa mashindano ya Umitashumta na Umiseta wamewataka wakazi wa mkoa wa Mtwara kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kufuatia mkoa huo kuwa wenyeji wa mashindano hayo ili kujiunua kiuchumi.

Mashindano hayo yanahusisha wanafunzi wa shule za sekondari na msingi yanatarajia kuanza Juni 8- Julai 7 mwaka huu.

Akizungumza leo Ijumaa, Aprili 19, 2019 kiongozi mkuu wa kamati tendaji ya Taifa ya maandalizi, Leonard Thadei amesema jiji la Mwanza wanalia kutokana na mashindano hayo kutoendelea kufanyika mkoani humo.

Amesema mkoa wa Mtwara baadhi ya huduma ni ngumu kutokana na Jiografia yake na hivyo wanatakiwa kujipanga ili waendelee kupata fursa za kuwa wenyeji wa mashindano hayo.

“Wananchi wote wameshirikishwa na namna ambavyo wanashiriki katika kutoa huduma, Mtwara tunajua baadhi ya huduma ni ngumu sana kutokana na jiografia yake lakini tunadhani mkijipanga vizuri inawezekana siku hiyo mgeni rasmi akaja akasema na mwaka ujao mchezo utafanyika hapa hapa,”amesema Thadei

Afisa elimu mkoa wa Mtwara, Germana Mung’oho amesema katika mashindano hayo watakuwa na wanafunzi zaidi ya 7,000 na maafisa zaidi ya 900.

“Fursa hii ni kubwa, si kwamba tu watu watakuja kujifunza michezo inavyofanyika na burdani,lakini pia ni fursa ya kiuchumi kwasababu wote hawa watakaofika watatumia vitu ambavyo viko Mtwara, niwaombe wanamtwara mchangamkie fursa hii vizuri,”amesema Mung’oho

Kaimu katibu Tawala mkoa wa Mtwara, Elias Nyabusani amesema kama mkoa wamejiandaa vyema kuwapokea wageni wote.