Mtoko wa Arsenal utakavyokuwa msimu ujao tema mate chini

Muktasari:

  • Kutokana na hilo, Arsenal haitakuwa na ujanja zaidi ya kuingia sokoni kufanya usajili katika dirisha la majira ya kiangazi na huu ndio mtoko wa kocha Emery utakavyokuwa kwa msimu ujao baada ya kuwanasa wakali anaowataka watue kwenye timu yake. Mtoko wa Emery kwa msimu ujao utakuwa wa 4-2-3-1.

LONDON,ENGLAND.ARSENAL imemaliza namba tano kwenye Ligi Kuu England kwenye msimu wake wa kwanza kocha Unai Emery. Kwa maana hiyo imeshindwa kukamatia tiketi ya kucheza UCL.

Kama watawachapa Chelsea kwenye fainali ya Europa League. Mambo hayo Kocha Emery hataki yatokee kwa msimu ujao. Kwenye dirisha lile la Januari hakuwa na pesa wa kufanya usajili wa maana na matokeo yake aliishia tu kumbeba kwa mkopo Denis Suarez kutoka Barcelona.

Kutokana na hilo, Arsenal haitakuwa na ujanja zaidi ya kuingia sokoni kufanya usajili katika dirisha la majira ya kiangazi na huu ndio mtoko wa kocha Emery utakavyokuwa kwa msimu ujao baada ya kuwanasa wakali anaowataka watue kwenye timu yake. Mtoko wa Emery kwa msimu ujao utakuwa wa 4-2-3-1.

Bernd Leno, kipa

Amekuwa na msimu wa kwanza mzuri huko Arsenal, akibeba vyema mikoba ya Petr Cech. Bila shaka Leno atakuwa mtu muhimu kwenye kikosi cha Arsenal kwa ajili ya kufikia malengo msimu ujao.

Hector Bellerin,beki wa kulia

Alikosa sehemu kubwa ya msimu huu kutokana na kuwa majeruhi, lakini bila shaka atarudi kwa haraka sana kwenye kikosi hicho atakapokuwa fiti. Bellerin ni muhimu kwa sababu anaisaidia timu kwenye mashambulizi.

Sead Kolasinac, beki wa kushoto

Kolasinac ni kipenzi cha kocha huyo na hasa mtindo wake wa kupanda mbele kushambulia huku akitambua majukumu yake ya kukaba.

Laurent Koscielny,beki wa kati

Beki bora kabisa wa kati wa Arsenal na bila shaka ataendelea kubaki kwenye kikosi hicho akitamba kwenye nafasi hiyo. Umri unakwenda kwa kasi kwake, lakini hakuna ubishi Emery hatakuwa na chaguo jingine zaidi ya Koscielny msimu ujao.

Samuel Umtiti,beki wa kati

Beki huyo wa Barcelona hana mpango wa kuondoka kwenye timu hiyo, lakini hakuna ubishi kwa msimu ujao hatakuwa na nafasi ya kucheza huko Nou Camp hasa kama watafanikiwa kumnasa mtu wao wanayemsaka, Matthijs de Ligt. Emery atajibebea Umtiti.

Lucas Torreira,kiungo wa kati

Moja ya majina ya kwanza katika kikosi cha Emery kwa siku za karibuni. Bila shaka kiungo Torreira ataendelea kubaki kwenye nafasi hiyo kwa msimu ujao na kuifanya timu kuwa na uimara zaidi kwenye mechi zake.

Dennis Praet,kiungo wa kati

Waliwahi kucheza pamoja huko Sampdoria na kuunda kombinesheni moja matata kabisa. Preat anatajwa kuwa mchezaji atakayekuja kuchukua mikoba ya Aaron Ramsey huko Emirates.

Mesut Ozil, kiungo mshambuliaji

Si kwamba muda wote Emery na Ozil wamekuwa hawaelewani, kuna nyakati nyingine wawili hao wanakuwa vizuri tu hasa staa huyo anapofanya mambo yake ndani ya uwanja. Hakuna ubishi, Ozil atakuwa kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal msimu ujao.

Pierre-Emerick Aubameyang, mshambuliaji

Aubameyang atakuwa akishambulia kutokea upande wa kushoto kitu ambacho amekifanya mara kadhaa msimu huu na kushinda Kiatu cha Dhahabu kwenye Ligi Kuu. Auba atatumika kama kiungo wa kushoto.

Ryan Fraser,mshambuliaji

Winga wa Bournemouth amekuwa na msimu bora na kinachotajwa ni kwamba atakwenda kujiunga na Arsenal. Kwenye timu hiyo ya Arsenal kama atatua, msimu ujao Fraser atashambulia kutokea upande wa kulia ambapo atatumika kama kiungo wa kulia.

Alexandre Lacazette, straika

Straika huyo wa Kifaransa amekuwa akizivutia timu nyingi ikiwamo Barcelona zinazohitaji saini yake. Lakini, kocha Emery hawezi kukubali kirahisi kuipoteza huduma ya mchezaji wake huyo.