Mtibwa Sugar tayari kimataifa

Muktasari:

Mbali na Mtibwa Sugar timu nyingine za ukanda wa Afrika Mashariki zinazoshiriki Kombe la Shirikisho ni pamoja na Zimamoto ya Zanzibar, Uganda ni KCCA, Burundi itawakilishwa na Vital'O, kwa Kenya ni Kariobangi Sharks na Rwanda ni Mukura Victory Sports.

KIKOSI cha Mtibwa Sugar kimetaja wachezaji 26, watakaoiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Kocha Mkuu, Zubery Katwila amesema hana wasiwasi na mashindano hayo.
Mtibwa Sugar ndiyo timu pekee kutoka Tanzania itakayocheza mashindano hayo kwa mujibu wa kanuni baada ya kuwa mabingwa wa Kombe la FA msimu uliopita.
Wachezaji hao ni Shaaban Kado, Benedictor Tinocco, Aboutwalib Mshery, Ally Shomary, Salum Kanon, Issa Rashid, Hassan Mganga, Dickson Daud, Dickson Job na Hassan Isihaka.
Wengine ni Shaaban Nditi, Henry Joseph, Saleh Khamis, Awadh Juma, Ally Makarani, Ayoub Semtawa, Salum Kihimbwa, Ismail Mhesa, Haruna Chanongo, Nassor Seif na Jaffary Kibaya.
Wapo pia, Juma Liuzio, Stamil Mbonde, Kelvin Sabato, Rifat Khamis, Cassian Ponera.
Katwila amesema, yuko tayari kwa ajili michuano hiyo: "Kila kitu kiko sawa. Wakati tunafanya maandalizi ya mechi za Ligi Kuu pia tulikuwa tunafanya na hayo ya Shirikisho kwa upande wangu kila kitu kipo tayari."
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Mtibwa Sugar, Salum Mayanga amesema: "Maendeleo mazuri kama klabu tulikuwa na mpango wa kucheza mechi tatu za kimataifa za kirafiki, tunaendelea kufanya mpango huo ili tuweze kukamilisha."
Mlinda mlango wa kikosi hicho, Tinocco amesema: "Sisi kama wachezaji tuko tayari kwa mashindano hayo na hakuna kitu kitakachoharibika."
Michuano hiyo mikubwa Bara la Afrika inatarajiwa kuanza rasmi Novemba 27, lakini mpaka sasa ratiba ya CAF bado haijatoka.
Wakati Simba yenyewe itaiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba ndiyo waliiwakilisha Tanzania msimu uliopita katika mashindano ya Kombe la Shirikisho na Yanga ilicheza Ligi ya Mabingwa Afrika.