Mtibwa, Coastal Union zatangaziana ubabe

Muktasari:

  • Wakati Coastal Union wakishika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu na pointi zao 47 wakati Mtibwa wako nafasi ya 14 wakiwa na pointi 33.

KOCHA Mkuu wa Mtibwa Sugar, Zuber Katwila amewataka wachezaji wake kupambana kuhakikisha wanashinda mchezo wa kesho ugenini dhidi ya Coastal Union huko Tanga.

Mchezo huo ni wa kwanza kwa Mtibwa Sugar kwenye Ligi Kuu tangu iliporejea Juni 13 wakati kwa Coastal Union utakuwa ni wa pili baada ya ule dhidi ya Namungo FC ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Akizungumza na Mwanaspoti Katwila amesema, anakubali kiwango cha wapinzani wao ila amewataka wachezaji wake kuzitumia vyema dakika 90 za mchezo huo.

"Mimi kama kocha nishamaliza kazi yangu, sasa imebakia kwa wao wachezaji kuhakikisha wanapambana kupata matokeo katika mchezo huo na mingineyo,"

Aidha Katwila anasema ana imani na vijana wake wote waliopo ndani ya kikosi chake, na kila mchezaji ana haki ya kucheza kwa kuwa kasajiliwa ndani ya kikosi hicho.

Katwila anasema, katika maandalizi yake ya kujiandaa na mechi zilizosalia za ligi walicheza  mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Kagera Sugar uliochezwa katika Uwanja wa  Manungu mkoani  Morogoro ambao  timu yake iliibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Anasema mchezo huo ulikuwa mzuri na wenye ushindani ambao ulimfanya  kupata mwanga wa kiwango cha  vijana wake licha ya kuhitaji mechi zaidi ya hiyo moja ila kutokana na muda kubana alishindwa kupata mechi nyingine.

Mtibwa Sugar katika msimamo wa Ligi inashika nafasi ya 14 ikiwa na pointi 33 baada ya kushinda michezo nane, sare tisa na kupoteza michezo 12 huku Coastal ikishika nafasi ya tano ikiwa na pointi 47 wakishinda michezo 13 sare nane na kupoteza michezo nane.

Kwa upande wake kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda amesema, anahitaji matokeo ya ushindi katika uwanja wao wa nyumbani ili kuzidi kujiweka katika nafasi nzuri kwenye  msimamo wa Ligi hiyo.

Mgunda anasema anaheshimu uwezo wa wapinzani wake kuelekea mchezo huo wa kesho kila atahakikisha wanapambana pointi zote tatu zibaki nyumbani.

"Mchezo uliopita tulipoteza pointi na kuambulia sare sasa huu wa kesho vijana nimewaambia wajitume wapate pointi zote tatu,"