Mtanzania afuzu majaribio timu ya Ligi Kuu Oman

Muktasari:

Msimu uliopita Hamis akiwa na Bandari alitwaa kombe la washindi wa pili kwenye Ligi hiyo ambapo walimaliza nyuma ya Gor Mahia ambao walichukua ubingwa wa msimu huo.

BAADA ya kufanya majaribio ya wiki kadhaa nchini Oman, hatimaye kiungo wa Kitanzania, Hamis Abdallah amefuzu majaribio hayo kwenye klabu ya Al-Nahda.

Hamis  ambaye alikuwa akiichezea Bandari ya Kenya, amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Oman ambayo ni maarufu kama Professional Ligi.

Mara baada ya kusaini mkataba huo, Hamis alisema vigogo wa chama hilo, wamempa nyumba ambayo ataishi kipindi chote atakachokuwa anaichezea Al-Nahda.

“Nilijiwekea malengo nilipokuwa Kenya, nimecheza kwa kipindi kirefu na hata kuitwa kwangu timu ya taifa kipindi cha Salum Mayanga ilitokana na Ligi yao, asanteni sana ambao walikuwa sehemu ya mimi kuwa na msingi mzuri wa soka.

“Umefika muda wa kuanza maisha yangu ya soka kwingine sina cha kuwalipwa jamaa na ndugu zangu wa Bandari na wengineo zaidi ya kusema asante kwa maisha tuliyoishi pamoja kama familia,” alisema Hamis.

Kiungo huyo, alisema anaitakia kila la kheri Bandari kwenye harakati ambazo walizianza pamoja za kuupigania ubingwa wa Ligi Kuu Kenya.

“Nachoweza kusikitika ni kwamba nimeondoka Kenya bila ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini humo lakini ninafuraha kuiacha timu kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa huo,” alisema.