Mtanuna mpasuke!

Friday April 26 2019

 

By SADDAM SADICK nA MASOUD MASASI, MWANZA

HUKO Jangwani watu wamenuna. Wamenuna kwa sababu kila wakihesabu alama walizonazo timu yao ya Yanga na kasi waliyonayo Simba inawakata stimu. Simba jana Alhamisi kwa mara nyingine tena walikula kiporo chao kibabe baada ya kuifumua KMC katika mechi ya Ligi Kuu Bara iliyopigwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Simba ikitoka kuibwaga Alliance mapema wiki hii kwenye uwanja huo huo kwa kuwafunga mabao 2-0, imepunguza pengo la pointi kati yao na Yanga kutoka 11 hadi kuwa nane, lakini wakiishusha Azam waliokuwa nafasi ya pili kwa tofauti na uwiano wa mabao ya kufunga na kufunga.

Ushindi wa jana ambao haukupokewa kwa vishindo na mashabiki kwa jinsi KMC walivyoibana Simba kwa dakika zote 90 za mchezo huo, umewafanya watetezi hao wa Ligi Kuu kufikisha alama 66 baada ya kucheza mechi 26, alama zilizowafanya walingane na Azam iliyocheza mechi 32.

Hata hivyo, Simba imepanda nafasi ya pili wakipishana na wapinzani wao hao, kutokana na kutofautiana mabao ya kufunga na kufungwa, Simba ikiwa na uwiano wa mabao 44 dhidi ya 30 ya Wana Lambalamba ambao Jumatatu wanatarajiwa kuvaana na Yanga iliyopo kileleni na pointi zao 74.

Simba imefunga jumla ya mabao 55 na kuruhusu 11, huku Azam ikiwa na mabao 49 ya kufunga na kufungwa 19 na kuzidi kufanya mbio za ubingwa msimu huu kuanza upya baina ya timu tatu za juu.

Katika mchezo wa jana uliokuwa mkali, Simba ilitangulia kupata bao katika dakika ya 23 kupitia kwa Emmanuel Okwi baada ya kuwahi mpira wa faulo, James Kotei na shuti lake kushinda nguvu kipa wa KMC, Jonathan Nahimana.

Advertisement

Bao hilo lilikuwa la 10 kwa Okwi msimu huu na la tatu mfululizo katika mechi tatu ambazo timu yake imecheza ikiwamo dhidi ya Coastal Union, Kagera Sugar na hiyo ya jana ya KMC ambayo ilicharuka baada ya bao hilo, lakini umakini mdogo wa washambuliaji wake uliwanyima bao la kusawazisha.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kushambuliana huku KMC wakimtumia winga wake, Hassan Kabunda aliyekuwa mwiba kwa ngome ya Simba na jitihada zao zilizaa matunda baada ya Kabunda kufunga bao la kusawazisha baada ya beki Zana Coulibaly kujichanganya kumpora mpira wakati akienda kumsalimia kipa Aishi Manula aliyepishana na shuti la winga huyo.

Bao hilo lilitinga nyavuni katika dakika ya 56 kabla ya Simba kupata penalti dakika chache baadaye kufuatia Okwi kumnawisha beki wa KMC mpira langoni mwake, lakini Meddie Kagere alikosa baada ya kipa Nihamana kuudaka. Kabla ya kupigwa kwa penalti hiyo wachezaji wa KMC walimzonga mwamuzi Abdallah Kambuzi wakiamini amewaonea kutoa adhabu hiyo.

Katika kipindi hicho Simba ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Kotei, Okwi na Clatous Chama ili kuwapisha Mzamiru Yasin, Hassan Dilunga na Mohammed ‘MO’ Ibrahim, mabadiliko yaliyoisaidia kupata bao la pili katika dakika ya 82 baada ya Mzamiru kumnawisha mpira Masoud Abadllah na mwamuzi kuamuru penalti iliyolalamikiwa na KMC kabla ya kutulia na John Bocco kuitupia nyavuni likiwa bao lake la 12 msimu huu. Dakika chache kabla ya kumalizika kwa pambano hilo James Msuva aliyeingia kipindi cha pili aliiwahi pasi ya nyuma ya Tshabalala kwa kipa wake, lakini akijiandaa kufunguka filimbi ilipulizwa akidaiwa kuotea, baada ya mshika kibendera Consolata Lazaro kunyanyua kibendera.

Tukio lilifanya mashabiki kuwazomea waamuzi hao, kwa maamuzi hayo wakionekana dhahiri wameshindwa kutafsiri sheria ya pasi ya kurudishiwa nyuma langoni (back pass), hata hivyo kelele hizo hazikusaidia kwani dakika 90 ziliimalizika kwa Simba kuibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Advertisement