Mtambo wa mabao Azam anarudi uwanjani Januari

Muktasari:

Mbaraka alipata majeraha ya goti akiwa anaichezea Namungo katika mechi za Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Azam anayecheza kwa mkopo Namungo, Mbaraka Yusuf atarejea uwanjani Januari baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu kutokana na majeraha ya goti.

Mbaraka alisema anaendele vizuri na matibabu ya goti na daktari wake amemwambia anaweza kurejea uwanjani kucheza soka la ushindani Januari kama hatapata shida tena nyingine yoyote.

"Nashukuru maendeleo yangu si mabaya napata matibabu mazuri huku uongozi wa Azam nikiwa nao pamoja katika kipindi hiki na matumaini yangu mpaka kufika Januari nitarudi tena uwanjani kucheza, nimeanza mazoezi mepesi," alisema Mbaraka.

Mbaraka alisajiliwa na Azam msimu wa 2017-18, baada ya kufunga mabao 12 akiwa na kikosi cha Kagera Sugar, lakini alishindwa kupata namba ya kudumu katika kikosi cha kwanza ndipo alipotolewa kwa mkopo Namungo ya Ligi.

Akiwa Namungo mshambuliaji huyo alisaidia timu hiyo kupanda Ligi Kuu kutokana na mabao yake kabla ya kuumia goti.