Msuva ni maajabu tu ughaibuni

Muktasari:

  • Kwa msimu wa pili mfululizo, Msuva amekuwa akitegemewa na Difaa kwenye ufungaji na msimu huu ni kinara wa mabao kwenye klabu hiyo huku akishika nafasi ya pili kwenye Batola Pro, kutokana na mabao yake 13.

NYOTA wa zamani wa Yanga, Saimon Msuva anayeichezea Difaa El Jadida, anasubiri maajabu siku ya kufunga pazia la Ligi Kuu Morocco pengine timu yake inaweza kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

Difaa ipo nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu Morocco ‘Batola Pro’,ikiwa na pointi 39 ambazo imejikusanyia kwenye michezo 29.

Msuva alisema pamoja na kuwa bado wana nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho msimu ujao, lakini kuambulia pointi moja kwenye mchezo uliopita dhidi ya Hassania Agadir kumewaweka pabaya.

“Huku kwetu timu ambayo inamaliza nafasi ya kwanza hadi ya pili inapata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, nafasi ya tatu ni Kombe la Shirikisho.

“Tupo nafasi ya sita, tuna pointi 39, Hassania Agadir tuliocheza nao wapo nafasi ya tatu wakiwa na pointi 42 kwa hiyo tunatakiwa kushinda mchezo wetu wa mwisho huku tukisikilizia matokeo ya wenzetu,” alisema.

Kwa msimu wa pili mfululizo, Msuva amekuwa akitegemewa na Difaa kwenye ufungaji na msimu huu ni kinara wa mabao kwenye klabu hiyo huku akishika nafasi ya pili kwenye Batola Pro, kutokana na mabao yake 13.

Vinara wa mabao kwenye ligi hiyo ni Lajour Mouhssine wa Raja Casablanca na Laba Kodjo wa Berkane wenye mabao 18 kila mmoja huku Msuva na Boua Koffi wa Olympique de safi wakifungana kwa mabao.

Pazia la ligi hiyo, linatarajiwa kufungwa Mei 25 kwa chama la Msuva kucheza na Raja Casablanca (52), ambayo imeutolea macho ubingwa wa msimu huu ikiwa imepisha na vinara wa ligi hiyo, Wydad Casablanca (55) kwa pointi tatu.