Msuva atoboa siri ya ushindi Stars

Muktasari:

Msuva anayecheza soka ya kulipwa katika Klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco, alisema wachezaji wote wameandaliwa kisaikolojia kukabiliana na mchezo ulioshika tiketi ya kuamua.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ Saimon Msuva, amesema aina ya mafunzo wanayopata Afrika Kusini yanatoa taswira ya kufanya vizuri katika mchezo wa Jumapili dhidi ya Lesotho.

Akizungumza kwa simu jana, Msuva alisema moja ya mafunzo wanayopata kwa Kocha Emmanuel Amunike ni kukabiliana na mchezo wa presha timu inapokuwa ugenini.

Msuva anayecheza soka ya kulipwa katika Klabu ya Difaa El Jadida ya Morocco, alisema wachezaji wote wameandaliwa kisaikolojia kukabiliana na mchezo ulioshika tiketi ya kuamua.

“Kikosi chetu kina wachezaji wengi ambao wamekomaa wana uwezo wa kukabiliana na presha ya mechi za ugenini, tuna kila sababu ya kuifunga Lesotho hata kama wapo nyumbani kwao,” alisema Msuva.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, alisema wataingia uwanjani kucheza soka ya kushambulia ili Lesotho wafunguke hatua inayoweza kuwapa fursa ya kufunga mabao.

Pia, Msuva alisema anaamini nafasi ya nahodha Mbwana Samatta inaweza kuzibwa na mchezaji aliyeandaliwa ingawa nyota huyo wa Klabu ya KRC Genk ya Ubelgiji, alitakiwa awepo katika mchezo huo.

Akizungumzia matokeo ya sare ya bao 1-1 iliyopata Taifa Stars katika mchezo wa awali, alisema udogo wa Uwanja wa Azam Complex ulichangia kutoa nafasi kwa Lesotho kupata bao la ugenini.

Msuva alisema Lesotho ilicheza kwa kujilinda na udogo wa Uwanja wa Chamazi uliwafanya watekeleze vyema mbinu za kujilinda katika mchezo huo uliopigwa Julai 7.

Wadau wa soka la Tanzania, wamezungumzia utofauti wa urefu na upana wa viwanja vya soka unavyoweza kutumika kama nyenzo ya kupata matokeo nyumbani au ugenini.

“Eneo la kuchezea likiwa dogo ni kawaida huwa inahitajika mbinu za ziada ili kupata ushindi, vinginevyo timu inayoshambulia muda wote inaweza kupoteza kama wanaozuia watashambulia kwa kushitukiza,” alisema nyota wa zamani wa Simba Boniface Pawasa.