Msuva apiga mbili Morocco

Monday April 16 2018

 

By Eliya Solomon

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Kimataifa wa Tanzania,  Saimon Msuva amefunga mabao mawili usiku kuamkia leo na kuisaidia klabu yake ya Difaa El Jadida kulazimisha sare ya mabao 3-3 na Khouribga katika mchezo wa Ligi Kuu Morocco.

Mabao hayo yamemfanya mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, kufikisha jumla ya mabao nane katika ligi ya nchi hiyo maarufu kama Batola Pro.

Akizunguza nasi mara baada ya mchezo huo kumalizika, Msuva alisema ilibidi wafanye kazi ya ziada ili kuambulia pointi hiyo moja baada ya kutanguliwa mabao mawili.

"Tulitangulia kupata bao la kuongoza, lakini jamaa wakapindua matokeo mpaka kipindi cha pili wakawa wanaongoza wao mabao 3-1, nilifunga bao la pili kwetu na tatu kwa Penalti," alisema Msuva.

Sare hiyo imeifanya Difaa wenye pointi 38 kuwa nafasi ya nne kwenye msimamo wa Batola Pro,  wakizidiwa pointi  tisa na vinara wa ligi hiyo, Ittihad Tanger.