Mrithi wa Manji kwa Laki mbili tu

Muktasari:

Viongozi wa Yanga jana Ijumaa walianika gharama za fomu za wagombea kwa kusema watakaopenda kuwania Uenyekiti ambao upo wazi baada ya Manji kujiuzulu Mei 20 mwaka jana na Makamu wa Rais nafasi iliyoachwa wazi na Clement Sanga watalazimika kulipia Sh 200,000 tu.

Dar es Salaam.HATIMAYE Yanga wamekubali kiroho safi kuachana na ishu za Yusuf Manji, baada ya mabosi wa klabu hiyo kuafikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kufanya uchaguzi Januari 13, huku mrithi wa bilionea huyo atapatikana kwa Sh 200,000 tu.
Viongozi wa Yanga jana Ijumaa walianika gharama za fomu za wagombea kwa kusema watakaopenda kuwania Uenyekiti ambao upo wazi baada ya Manji kujiuzulu Mei 20 mwaka jana na Makamu wa Rais nafasi iliyoachwa wazi na Clement Sanga watalazimika kulipia Sh 200,000 tu.
Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, Tobias Lingalangala alisema nafasi ya Ujumbe kila mgombea atatoka kiasi cha Sh 100,o00 tu na fomu zimeanza kutolewa rasmi.
Lingalangala aliyeambana na viongozi kadhaa wa TFF akiwemo Kaimu Mkurugenzi wa Sheria wa shirikisho hilo, Rahim Shaaban, alisema;
"Vituo ni viwili ambavyo vitatumika kwa wanaohitaji kuiongoza Yanga kujichukulia fomu, vituo hivyo ni hapa TFF na kingine ni makao makuu ya klabu yetu na pesa zote za fomu hizo zitalipwa benki."
Naye Kaimu Mkurugenzi wa sheria wa TFF, Shaaban alitoa ufafanuzi siku tano tu zilizopo kwa wenye nia ya kuiongoza Yanga wanaweza kuzitumia kuchukua fomu.
“Hakuna ratiba ambayo inaweza kubadilika kila kitu kiko wazi na tutaweka miongozo mingine, miongozo hiyo tutabandika hapa na Yanga nasikia kwao wameshaweka,” alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti hiyo, Yusuf  Manji aliandika barua ya kujiuzuru nafasi hiyo Mei 20 mwaka jana ambapo hajaonyesha nia ya kurejea hata pale alipofuatwa kuombwa ili aendelee kuiongoza Yanga.

TAMKO KESHO
Hata hivyo wakati Lingalangala na viongozi wa TFF wakisisitiza mchakato ndio umeanza rasmi kuelekea kupata viongozi wa juu wa Yanga, habari za ndani kutoka klabu hiyo zinasema kuwa kesho Jumapili Baraza la Wadhamini litatoa tamko lao baada ya kuteta na Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga.
"Unajua Manji ameandika barua ya kurejea Yanga na viongozi walishatoa taarifa TFF, ila kuna hali fulani inafanyika kutaka kuivuruga klabu yetu, lakini bahati nzuri Baraza la Wadhamini litatoa tamko Jumapili na kuanika barua ya Manji," kilisema chanzo kutoka ndani ya Yanga kuonyesha bado kuna sintofahamu katika uchaguzi huo.
Hata hivyo Lingalangala alipoulizwa juu ya ishu hiyo na kikao cha kesho, alisema kwa ufupi: "Hakuna kikao chochote Yanga mpaka baada ya Uchaguzi Mkuu na lazima wajue kabisa serikali sasa ipo makini, watafuatilia chochote kitakachotokea kuelekea uchaguzi wa klabu yetu."