Mourinho kashtua kumpanga Pogba beki

Muktasari:

Kocha wa Manchester United, Jose Mourinho aliwashtua mashabiki na wadau wa soka baada ya kufanya uamuzi magumu ya kumchezesha kiungo Paul Pogba nafasi ya beki ya kati huku wakiwa nyuma kwa mabao 2-0, dhidi ya Newcastle United. Lakini mabadiliko hayo yalizaa matunda na kikosi cha Mashetani Wekundu hao wakaibuka na ushindi wa mabao 3-2.

MANCHESTER, ENGLAND. Kocha Jose Mourinho amewavuruga mashabiki wa soka duniani baada ya kuamua kumpanga Paul Pogba acheze beki juzi kwenye mechi dhidi ya Newcastle United na kuwafanya mashabiki hao kutumia kurasa zao za Twitter kuelezea mchangao wao.
Mourinho aliamua kumrudisha Pogba kwenye beki ya kati, wakati huo Man United ikiwa nyuma kwa mabao 2-0 katika mechi hiyo iliyofanyika uwanjani Old Trafford.
Lakini kitu kizuri kwa Mourinho ni kwamba mabadiliko yake yaliifanya Man United kutumia dakika 20 za mwisho kufunga mara tatu na hivyo kushinda mechi hiyo 3-2 na kuondoa presha ya Kocha Mourinho, ambaye amekuwa akitajwatajwa huenda angefutwa kazi kama angeshindwa kupata matokeo mazuri kwenye mechi hiyo.
Mourinho alimtoa beki wa kati Eric Bailly dakika ya 19 tu na kumwingiza Juan Mata, kisha baada ya kurudi kipindi cha pili, akamwingiza Marouane Fellaini kuchukua nafasi ya Scott McTominay.
Wakati kipindi cha pili kikiwa kinaanza, Mourinho alibadili mfumo na Pogba kurudishwa nyuma kwenye safu ya mabeki wa kati watatu, sambamba na Nemanja Matic na Chris Smalling. Mabadiliko hayo yaliyoleta matokeo chanya na Man United kushinda 3-2, shukrani kwa mabao ya Mata, Anthony Martial na Alexis Sanchez.
Shabiki mmoja kwenye Twitter, akiuliza kwani nini kinaendelea duniani baada ya kuona Mourinho anampanga Pogba beki wa kati, huku shabiki mwingine, ambaye wazi ni wa Liverpool, aliandika Man United iliwacheka waliposajili beki kwa Pauni 75 milioni, lakini wao yaani Man United, imenunua beki kwa Pauni 89 milioni, kwa maana ya Pogba.