Mourinho amshukuru muokota mipira

Muktasari:

Ushindi wa mabao 4-2 ambao Tottenham wameupata umewafanya kutinga hatua ya mtoano huku Mourinho akiweka rekodi ya kuwa kocha wa kwanza kutoka England kutinga hatua hiyo akiwa na timu tatu tofauti kutoka nchini humo.

London, England .KOCHA wa Tottenham,  Jose Mourinho amemwagia sifa muokota mipira uwanjani 'ball boy' kwa kuwa sehemu ya bao muhimu lililofungwa na Harry Kane katika mchezo wa jana Jumanne usiku  dhidi ya Olympiacos.

Wakati ambao Tottenham  walikuwa nyuma mabao 2-1, kijana muokota mipira, alifanya kwa haraka kumpa mpira uliokuwa umetoka, Serge Aurier.

Aurier naye alimrushia Lucas Moura wakati huo mabeki wakiwa wamezubaa, walistuka akiwa anapiga krosi iliyomaliziwa na Kane ambaye aliifungia Tottenham waliokuwa nyumbani bao la kusawazisha.

Baada ya kumalizika mchezo huo ambao Tottenham  waliibuka na ushindi wa mabao 4-2, Mourinho alisema, "Nimependa alichofanya yule kijana. Aliuelewa mchezo na kutoa msaada,".

Olympiacos walianza kuitangulia Tottenham  mabao mawili ya haraka yaliyofungwa na  Youssef El-Arabi na  Ruben Semedo kabla ya kujisawazishia katika mchezo huo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kupitia Dele Alli na  Kane.

Aurier aliifungia Tottenham  bao la tatu huku Kane akipachika na la nne.

Real Madrid na PSG ambao walitoka sare ya mabao 2-2 nao wamesonga mbele hatua ya mtoano licha ya kuwa wamebaki na mchezo mmoja mbele yao kabla ya kumalizika hatua ya makundi.

Vigogo wengine ambao wana tiketi ya kutinga raundi hiyo ni Juventus, Bayern Munich, PSG na Manchester City.

Kuna michezo mingine  inatarajiwa kuendelea leo ambapo Mbwana Samatta akiwa na KRC Genk watakuwa na kiburua kizito mbele ya Salzburg,  Liverpool ambao wapo nao kundi moja E, watacheza dhidi ya Napoli.

Michezo mingine ni Chelsea watacheza dhidi ya Valencia huku Barcelona ikicheza dhidi ya  Borussia Dortmund.