Mourinho alikataa kulipa zaidi ya Pauni 50 milioni kwa Maguire

Muktasari:

Mourinho alidai kwamba kumsajili Maguire kwa zaidi ya Pauni 50 milioni kwanza ni kumkosea tu adabu mchezaji mwenyewe kwa maana kwamba hana thamani hiyo.

MANCHESTER,ENGLAND.MANCHESTER United wamemfanya Harry Maguire kuwa beki ghali zaidi duniani. Walitumia Pauni 80 milioni kunasa saini yake kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi huko Ulaya.

Lakini, kama Man United ingekuwa bado ipo chini ya Jose Mourinho, Maguire angeisikilizia timu hiyo kwenye redio tu. Asingetua Old Trafford. Bahati nzuri kwa Maguire kwamba Old Trafford amekuja kocha mpya, Ole Gunnar Solskjaer na hilo limemfanya kuweka rekodi yake tamu duniani ya kuwa beki ghali, akivunja rekodi ya Virgil van Dijk.

Unaambiwa hivi, Maguire angetua Man United siku nyingi sana, lakini Mourinho ndiye aliyezuia uhamisho huo, kisa pesa kubwa.

Kocha huyo Mreno anayedaiwa kupenda kutumia pesa nyingi kwenye kununua wachezaji anaripotiwa kwamba aliwaambia mabosi wake kwamba thamani ya Maguire ni Pauni 50 milioni tu, wasilipe zaidi ya hapo.

Mourinho alidai kwamba kumsajili Maguire kwa zaidi ya Pauni 50 milioni kwanza ni kumkosea tu adabu mchezaji mwenyewe kwa maana kwamba hana thamani hiyo.

Mtu mmoja kutoka ndani ya klabu hiyo alisema: “Uhamisho wa Maguire ulipaswa kufanyika kwenye majira ya kiangazi 2018 kwa sababu Mourinho alikuwa amepitisha na kusema beki huyo asajiliwe.”

“Lakini, Jose aliweka masharti kidogo. Alisema Maguire ni mchezaji mzuri, lakini thamani yake haiwezi kuzidi Pauni 50 milioni.

“Akasema kulipa zaidi ya Pauni 50 milioni ni kumkosea mchezaji mwenyewe. Mabosi wa Man United wakawa wameambiwa hivyo. Lakini, Leicester wao walikuwa wameshapanga bei yao kwamba hawawezi kumuuza Maguire kwa dau lisilozidi Pauni 60 milioni.

“Dili likafa na Man United hawakupeleka ofa rasmi hadi hapo walipoamua kufanya hivyo mwaka uliofuatia huku thamani ya Maguire ikipanda zaidi na kusajiliwa kwa Pauni 80 milioni.”

Man United wamemfanya Maguire kuwa beki ghali duniani huku huduma yake huko Old Trafford bado ikionyesha mashaka makubwa kutokana na timu hiyo kuruhusu mabao 12 kwenye Ligi Kuu England msimu huu, huku mara kadhaa Muingereza huyo akionekana kuwa ni wa kawaida asiyestahili kununuliwa kwa pesa nyingi kiasi hicho.