Mourinho,Lampard watiana mikononi

Muktasari:

Wakati Mourinho akiongea hayo, Lampard alikuwa jeuri na kudai hakuwa na mpango wa kumsikiliza kocha huyo kwa lolote huku akiamini katika kile walichopanga kukifanya.

LONDON, ENGLAND . HAIKUWA siku nzuri kwa Chelsea juzi Jumapili pale Old Trafford. Ilipokea kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Manchester United katika pambano la kwanza la msimu baina ya timu hizo.

Pambano hilo halikuwaacha salama kocha wa zamani wa Chelsea, Jose Mourinho aliyekuwa mchambuzi katika Kituo cha Sky Sports na kocha wa sasa wa Chelsea, Frank Lampard ambaye ni staa wa zamani wa Chelsea katika utawala wa Mourinho.

Mourinho alikosoa uamuzi wa Lampard kuwaacha baadhi ya mastaa wa timu hiyo nje na kuwapanga wachezaji aliowaita wachanga ambao hawakuweza kukabiliana vyema na Manchester United katika uwanja wa ugenini Old Trafford.

Mourinho alishangazwa na kitendo cha Lampard kutomuanzisha kiungo wa kimataifa wa Ufaransa, N’Golo Kante hata kama staa huyo ndiye kwanza anarudi kutoka katika majeraha.

Lakini akashangazwa pia na kitendo cha Lampard kuwaacha nje Marcos Alonso na Olivier Giroud.

Kocha huyo Mreno aliyetwaa mataji manane katika vipindi vyake viwili Stamford Bridge alimshambulia zaidi Lampard kwa kudai timu yake ilikuwa laini na haikutumia sana nguvu huku ikishindwa kucheza kwa pamoja eneo la nyuma.

“Chelsea ilikuwa laini, haikujilinda kwa pamoja nyuma na haikutumia sana nguvu. Kulikuwa na nafasi kubwa sana kati ya wachezaji wa mbele na wale wa nyuma. Haikukaba katika kila eneo,” alisema Mourinho.

“Kama Kante anaweza kucheza dakika 30 au 35 basi anaweza kuanza mechi. Na kama akiweza kucheza kwa saa moja basi mwache acheze kwa saa moja. Lakini labda Frank anatusikiliza sisi na kusema Kante hawezi kucheza. Hisia zangu ni kwamba alikuwa na uwezekano wa kucheza.”

“(Marcos) Alonso alikuwa katika benchi, Kante alikuwa katika benchi, (Olivier) Giroud alikuwa katika benchi, na kama umekuja Old Trafford namna hiyo, hata kama sio Manchester United inayotisha kama ilivyozoeleka lakini bado inabakia kuwa Manchester United,” aliongeza Mourinho.

“Wachezaji wenye uzoefu wangeweza kucheza vyema zaidi. Unaangalia viwango vya Mason Mount, Tammy Abraham na kisha unapima, kwa wachezaji wa aina hii unahitaji nguvu kidogo. Kulikuwa na wakati ambapo Chelsea bila ya kuwa na mpira ungeweza kuona kuna makundi sita au manne uwanja tofauti. Abraham, Barkley, Pedro na Mount walibaki juu.”

“Timu nzuri zote zinakaba kwa pamoja, eneo la juu na eneo la chini. Kuna kanuni za mchezo ambazo ni lazima. Mnajilinda kwa pamoja. Chelsea kamwe haikufanya hivyo. Kwa hiyo mambo yalikuwa rahisi kwa United,” aliongeza kocha huyo.

Wakati Mourinho akiongea hayo, Lampard alikuwa jeuri na kudai hakuwa na mpango wa kumsikiliza kocha huyo kwa lolote huku akiamini katika kile walichopanga kukifanya.

“Sihitaji kuwaza sana kuhusu kitu kinachosemwa na mtu yeyote yule, wachambuzi, lakini ni wazi kwamba kikosi tulichonacho ndicho tulichanacho na nakiamini. Siwezi kulazimisha kuwapanga watu kutoka katika chumba cha matibabu haijalishi kama wana uzoefu au hawana. Wachezaji waliocheza leo na waliokaa benchi ndio wachezaji ambao tunao.

“Tunawakosa wachezaji wa kimataifa na wachezaji wakubwa, lakini sitaki hilo liwe kisingizio. Tulipambana kwa kipindi kirefu. Tulifnya makosa manne na walituadhibu.

“Ni angalizo kwetu. Sio kwamba matokeo ya 4-0 yalikuwepo kwa muda mrefu, lakini inabidi tukubali,” alisema staa huyo wa zamani wa kimataifa wa England.

Kabla ya kuanza kwa pambano hilo, tayari Mourinho alichafua hali ya hewa baada ya kudai timu ya Manchester B na wachezaji wa akiba wanaweza kushika nafasi ya nne katika msimamo mbele ya Manchester United, Arsenal na Chelsea.

Alipoulizwa kuhusu timu gani anaamini zitawania ubingwa alisema, “timu nne; Man City, Tottenham, Liverpool na timu B ya Manchester City. Nilipotazama benchi la Manchester City na wachezaji ambao hawakujumuishwa katika kikosi cha kwanza, naamini kwamba hata timu yao B inaweza kutwaa kombe.”

Hata hivyo Kocha Mourinho ambaye amewahi kuzinoa Chelsea na Man United alisisitiza Arsenal, Chelsea na Manchester United zinaweza kufanya maajabu huku akisema, “wakati mwingine katika soka mambo yasiyotabirika huwa yanatokea.”