Moto wao si mchezo EPL

Raundi ya pili imepigwa huko Ligi Kuu England na kwa sasa pale kwenye msimamo kinara ni Leicester City ikiwa na pointi sita sambamba na Everton inayoshika nafasi ya pili na Arsenal ya tatu zikitofautiana kwa mabao ya kufunga na kufungwa.

Hata hivyo, wakati utamu wa EPL ukiwa ndio kwanza umeanza, tayari kuna mashine huko hazitaki utani na wamekiwasha ile mbaya wakiendeleza moto wao wa msimu uliopita.

Mwanaspoti linakuletea mastaa 11 tu ambao wameanza na kasi na wakiendelea hivi, EPL itakuwa moto msimu huu.

11. Heung-Min Son- spurs

Ilikuwa ni kama kufuta machungu baada ya kuanza vipaya kwa kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Everton ya Carlo Ancelotti na kutibua mambo huko kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.

Hata hivyo, Tottenham ya Kocha Jose Mourinho haikutaka kurudia makosa na kupitia mshambuliaji wao raia wa Korea, Heung-Min Son ilimaliza hasira kwa Southampton kwa kuichapa mabao 5-2 ugenini. Kwenye mchezo huo alitupia mabao matatu ‘Hat trick’ na kuifanya Spurs itoke kibabe uwanjani.

10. Mateusz Klich - Leeds

Achana na kichapo cha mabao 4-3 kutoka kwa Liverpool ilichopata Leeds United kwenye mchezo wao wa kwanza Ligi Kuu England baada ya kuruejea tena, shughuli ilikuwa kwenye miguu ya nyota wao Mateusz Klich. Aliwahangaisha sana Liverpool kwenye mchezo huo kutokana na ufundi, ubabe, akili, pasi zake zenye macho, nguvu nyingi, pamoja na kasi yake na kutawala eneo la kiungo.

Mpoland huyu, kama ilivyokuwa dhidi ya Liverpool aliisaidia timu yake kuifumua Fulham mabao 4-3 kwenye mchezo wa pili kwenye uwanja wao wa Elland Roadakifunga bao moja la penalti na kutoa asisti moja.

9. Tariq Lamptey na Neal Maupey - Brighton

Kina anayekuja kwa kasi Tariq Lamptey (19) aliweza kupunguza mabao ya Chelsea ambao walikuwa anakuja kwa kasi langoni mwa mwa Brighton kwenye mchezo wao wa Jumatatu.

Beki huyu wa kulia alikuwa bora katika kufanya ‘tackle’ na kusukuma mashambulizi mbele, akitokea pembeni.

Kwa upande wa Neul Maupey alionyesha kiwango bora kwenye mchezo wa pili dhidi ya Newcastle United akiisaidia Brighton kushinda mabao 3-0, akitupia wavuni mara mbili na kutoa asisti ya bao la tatu.

8. Wilfried Zaha - Crystal Palace

Kinachowafurahisha mashabiki wa Palace ni mkali wao huyu hafikirii kabisa kuondoka pale Selhurst Park.

Wanaifahamu shughuli yake na katika kudhihiriha hilo, kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya Sauthampton aliisaidia timu yake kushinda bao 1-0 akitoa asisti ya bao lililofungwa na Alex McCarthy ambalo likikataliwa na VAR.

Moto

aliuongeza kwenye mchezo wao wa pili Jumamosi dhidi ya Manchester United ikishinda mabao 2-1, Old Trafford akiwapa tabu mabeki wa United hasa Lindelof.

Zaha alifunga mabao mawili, katika dakika ya 74 na 85, na kuiongoza Palace kuitandika United 3-1.

7. Pierre-Emerick Aubameyang – Arsenal

Kasi yake msimu huu si ya mchezo, baada ya kuisaidia Arsenal kutwaa mataji mawili, lile na Ngao ya Jamii dhidi ya Liverpool na Kombe la FA, Aubameyang anazidi tu kutisha.

Tayari ameshasaini mkataba mpya na Arsenal kabla ya Jumamosi kuanza kufanya mavitu yake dhidi ya Fulham.

Akipokea mpira kutoka winga ya kushoto alikokuwa Mbrazil Willian, Auba alikatiza hadi katikati mwa dimba, akitumia guu lake la kulia, akaachia shuti lililoenda moja kwa moja wavuni na kudhihirisha amepania kulibeba chama la Kocha Mhispania Mikel Arteta anayewapa furaha mashabiki wa timu hiyo kwa sasa.

6. Jamie Vardy – Leicester

Alitupia mabao mawili kwenye mchezo wao wa kwanza dhidi ya West Bromwich kwenye ushindi wa mabao 3-0 wikiendi iliyopita.

Amekuwa ndio alama ya Leicester na shughuli ya kutupia ni rahisi kwake baada ya kumaliza msimu uliopita kinara wa mabao akiwa nayo 23.

5. Reece James - Chelsea

Amekuwa moto wa kuotea mbali kwenye kikosi Chelsea na nguzo muhimu katika safu ya beki ya kulia.

Jumatatu, dhidi ya Brighton alionyesha kiwango kikubwa akipandisha mashambulizi akifunga pia bao la shuti la mbali na kuchangia bao Kurt Zouma,kwenye Uwanja wa AMEX. Alipiga shughuli kubwa kwenye eneo lake la beki, akihusika zaidi ya mara moja, kufuta mipango ya Brighton.

4. Calvert Lewin- Everton

Kwenye michezo yote miwili Dominic Nathaniel Calvert-Lewin (23) alionyesha kiwango kizuri na alifanikiwa kufunga mabao matatu ‘Hat trick dhidi ya West Brom kwenye ushindi wa mabao 5-2, ugani Goodison Park, Jumamosi.

3. Gabriel Magalhaes - Arsenal

Kama kuna tatizo ambalo limekuwa likimsumbua Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, basi ni eneo la beki. Hata hivyo, kwa kiwango kilichoonyeshwa na sajili mpya, Gabriel Magalhaes dhidi ya Fulham hakikuwa cha kitoto kabisa baada ya kuonyesha tatizo la beki sasa limepungua kama sio kwisha kabisa..

Katika mchezo ule, ukiachilia bao lake, pia alionyesha utulivu wa hali ya juu. Alikuwa ngangari, akiwahakikisha wanaondoka Craven Cottage kifua mbele.

2. Willian - Arsenal

Mbrazil huyo alikuwa moto wa kuotea mbali kwa mabeki wa Fulham. Alitoa asisti mbili, bao la Aubemayang na Gabriel.

Alitengeneza kombinesheni matata na, Aubameyang na Alexandre Lacazette. Muda sio mrefu, Dunia itasahau kama, Willian aliwahi kuichezea Chelsea.

1. Mohamed Salah na Sadio Mane- Liverpool

Ubora wao uliisaidia Liverpool kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na taji la EPL na msimu huu, Salah alianza shughuli yake kwenye ushindi wa mabao 4-3 dhidi ya Leeds United, Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Anfield.

Katika mchezo huo, Salah alifunga hat-trick ya kwanza ya msimu wa 2020/21 wa ligi kuu ya England (EPL). Juzi Jumapili katika mechi yao ya pili kwenye Stamford Bridge, Sadio Mane naye alipokea kijiti na kuiongoza Liverpool kuitandika

Chelsea 2-0, akitupia kambani katika dakika ya 50 na 54.