Morrison rasmi Simba

Muktasari:

Uongozi wa Yanga hivi karibuni ulikaa kikao kizito na wachezaji wao, kiliamua kuwaacha baadhi, wengine kuwabakisha akiwemo Morrison, wakisisitiza ni mchezaji wao.

HAYAWI hayawi sasa yamekuwa, ile hadithi ya winga Benard Morrison kutua Simba imefika  mwisho baada ya leo kutangazwa kuitumikia klabu hiyo msimu ujao.
Yanga ilitangaza kwamba Morrison ni mchezaji wao akiwa na mkataba mpya wa miaka miwili, lakini mchana huu Simba imemtangaza staa huyo kupitia mtandao wao wa kijamii (Instagramu), wakiweka picha yake akiwa amevalia uzi wa jezi nyekundu, huku akionekana kumwaga wino kwa bashasha.
Mabishano hayo yamefika mwisho kuelewa Morrison atakuwa timu gani katika msimu ujao, kama tetesi ambazo zilikuwepo tangu mwanzo kwamba amesaini Simba na imethibitika hivyo leo Jumamosi ya Agosti 8.
Uongozi wa Yanga hivi karibuni ulikaa kikao kizito na wachezaji wao, kiliamua kuwaacha baadhi, wengine kuwabakisha akiwemo Morrison, wakisisitiza ni mchezaji wao.
Afisa Habari wa timu hiyo, Hassan Bumbuli alikaririwa kwamba "Morrison ni mchezaji wetu halali na hatujamuacha kama anabisha akasaini timu yoyote."
Katika ukurasa wa mtandao wa kijamii (Instagramu), hawajaandika mbwembwe nyingi kilichoandikwa ni 'Morrison is red', kumaanisha kwa sasa Mghana huyo naye ni Mwekundu wa Msimbazi.
Mapema jana Kigogo wa GSM, Hersi Said alinukuliwa na Mwanaspoti wanasubiri Simba imtambulishe Morrison ili wawape fedha na kuwashusha daraja kwani ni mali yao na pia walifanya kosa kubwa la kuzungumza naye na kumpa fedha akiwa ndani ya mkataba wao wa awali.
Morrison alisajiliwa na Yanga kwenye dirisha dogo na kuifungia mabao manne katika Ligi Kuu Bara ikiwamo lile lililowalaza mapema mashabiki wa Simba katika mechi iliyopigwa Machi 8.