Morrison atajwa kwenye usajili Sauzi

Muktasari:

Kocha huyo amedai kwamba kwa sasa mkakati wake mkubwa ni kuhakikisha timu yake inafanya vizuri katika Ligi Kuu na Kombe la FA.

KWA mujibu wa Gazeti kubwa la michezo la Afrika Kusini, Soccer Laduma, kocha wa Yanga, Luc Eymael na staa wa mashabiki, Bernard Morrison mambo yakienda freshi watarudi Sauzi.

Gazeti hilo limesisitiza kwamba Eymael yuko kwenye mazungumzo na klabu kadhaa na wanajua atarejea muda wowote ingawa mwenyewe amesisitiza ni uzushi na wanataka kumgombanisha na Yanga.

Taarifa hiyo ya gazeti hilo linaloaminika inasema kwamba Morrison anawindwa na Cape City na Black Leopards na ataungana na kocha wake kurejea Afrika Kusini ambako walishawahi kufanya kazi siku za nyuma na wanaelewana kwelikweli.

Hata hivyo, kocha huyo aliliambia gazeti hili kuwa ni uzushi tu. “Hakuna ukweli wowote kuwa najiandaa kuachana na Yanga. Namjua huyo aliyetoa hizo habari wala siyo wakala wangu, wanatoa vitu vya uongo na wanataka kunigombanisha na Yanga. Morrison yeye kama amezungumza nao sielewi, lakini ninachojua ni uzushi tu,”alisisitiza Kocha huyo mwenye uzoefu na Soka la Sauzi.

Kocha huyo amedai kwamba kwa sasa mkakati wake mkubwa ni kuhakikisha timu yake inafanya vizuri katika Ligi Kuu na Kombe la FA.

Kabla ya kujiunga na Yanga, Eymael alikuwa Afrika Kusini alikoifundisha Black Leopards lakini kabla ya hapo alizifundisha timu nyingine mbili za nchini humo ambazo ni Polokwane City na Free State Stars.