Morrison alikoroga tena Yanga

Muktasari:

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema, Morrison alikuwa kwenye mipango ya Kocha Eymael hasa kwa mchezo ujao wa Kagera Sugar na ule wa nusu fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Simba

WAKATI hatma ya kesi yake na Yanga ikitarajiwa kutolewa leo, imeelezwa winga Bernard Morrison amechomoa kusafiri na timu kwenda Kanda ya Ziwa, licha ya awali kuelezwa suala lake la kutoroka kambini limeshamalizwa na Kocha Luc Eymael naye kuomba msamaha na kujumuishwa mazoezini.

Habari kutoka ndani ya Yanga zinasema, Morrison alikuwa kwenye mipango ya Kocha Eymael hasa kwa mchezo ujao wa Kagera Sugar na ule wa nusu fainali ya Kombe la ASFC dhidi ya Simba, lakini ghafla mchezaji huyo ametakaa kuondoka na timu, huku taarifa nyingine ikielezwa alichomolewa na viongozi kwa kuhofia ataleta mpasuko.

Hata hivyo, Eymael alipoulizwa akiwa jijini Mwanza alisema hakuambatana Morrison na nahodha Papy Tshishimbi kutokana na matatizo mbalimbali, lakini hakutaka kufafanua zaidi juu ya suala la awali kuwepo kwenye mipango yake na kuchomoa kuondoka naye.

Yanga iliondoka janamchana kwa ndege kwenda Mwanza ikiwa safarini mkoani Mara kwa mechi ya kesho dhidi ya Biashara United na Morrison, licha ya sakata la kupelekana na mabosi wake ofisi za TFF, alishiriki mazoezi ya juzi kwa kilichoelezwa aliomba msamaha.

Taarifa nyingine kutoka ndani ya Yanga zinasema, licha ya Eymael kuonekana kulimaliza suala la Morrison kishkaji na kutaka kumjumuisha kikosini, mabosi wa klabu hakufurahishwa na kutaka aachwe ili asiwavuruge wenzake, kwani kwa aliyoyafanya anastahili adhabiwe.

Kabla ya kuibukia TFF, Morrison anadaiwa alitoroka kambini na kumtishia mlinzi kitu cha ncha kali hali iliyomfanya Eymael kumtimua, lakini ghafla juzi alizungumza naye na kudaiwa kutamaliza na kumpa ruksa kufanya mazoezini na kuingia kambini kwa safari ya mechi za Kanda ya Ziwa na ile ya Simba, lakini viongozi wanadai hawakuwa na taarifa juu ya mchezaji kusamehewa.

“Hakukuwa na mpango wa Morrison kusafiri na timu, pamoja na kuwa na taarifa ya kujumuika mazoezini na wenzake,” alisema Afisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli.

Morrison mwenyewe hakupatikana kufafanua juu ya kilichotokea, kwani simu yake iliita bila kupokewa, lakini ile kesi yake na Yanga kwenye ofisi za TFF juu ya kupinga taarifa ya kusaini mkataba mpya wa miaka miwili inatarajiwa kutolewa taarifa rasmi leo kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji, Elias Mwanjala.