Morice: Afcon ya vijana ni zamu yetu

Muktasari:

  • Moris ambaye alishindwa kuendelea na mazoezi na wenzake kutokana na kushtua kifundo cha mguu alisema wamejipanga kufanya vyema ili kutimiza malengo yao kama ilivyokuwa kwa kaka zao Stars, hasa wakiwa nyumbani.

NAHODHA wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, Morice Abraham amesema timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ wameanza wao watamaliza.

Kauli hiyo ameitoa siku moja baada ya Stars kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa kuifunga Uganda bao 3-0 na kuweka wazi ni mwanzo mzuri na wao wanakuja na mwendelezo wa kuweka historia katika nchi yao kuelekea mashindano ya Afcon kwa vijana yatakayoanza Aprili mwaka huu.

Moris ambaye alishindwa kuendelea na mazoezi na wenzake kutokana na kushtua kifundo cha mguu alisema wamejipanga kufanya vyema ili kutimiza malengo yao kama ilivyokuwa kwa kaka zao Stars, hasa wakiwa nyumbani.

Alisema wanatambua wanamlima mrefu lakini wamejipanga kwaajili ya kushindana na sio kukubali kushindwa “Hakuna aliyekuwa anatarajia Stars anaweza kumfunga Uganda juzi wamefanya hivyo kwanini sisi tushindwe,”

“Tuna kikosi kizuri tunaendelea na mazoezi huku kila mchezaji akiwa katika hari nzuri ya kupambana na kutamani kufanya vizuri kwaajili ya nchi watanzania tunaomba ushirikiano wenu tunaweza kufika mbali,”

“Nawapongeza Stars kwa mwanga waliotuonyesha na kutupa nguvu ya upambanaji hatutawaangusha tutafuata nyayo zao ili tuendelee kuwaweka Watanzania pamoja,” alisema.