Molinga akalia kuti kavu Yanga

Muktasari:

Molinga hadi sasa ana mabao manane katika orodha ya wafungaji inayoongozwa na Meddie Kagere wa Simba mabao 19, Yusuph Mhilu wa Kagera Sugar, Paul Nonga wa Lipuli na Reliants Lusajo wa Namungo kila mmoja ana mabao 11.

Dar es Salaam. Kinara wa mabao Yanga, mshambuliaji David Molinga siku zake ndani ya klabu hiyo zimeanza kuhesabika.

Mshambuliaji Molinga amefunga mabao manane hadi sasa katika Ligi Kuu Tanzania Bara, lakini maisha yake ndani Yanga yamekuwa njia panda tangu kutimuliwa kwa kocha Mwinyi Zahera.

Kocha Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amekabidhi ripoti yake akianisha wachezaji anaotaka kuwa nao kwa msimu ujao pamoja na wale wa kuachwa au kutolewa kwa mkopo.

Habari za ndani ambazo tovuti ya Mwanaspoti imepenyezewa kutoka kwa mmoja wa viongozi wa juu wa Yanga zilisema miongoni mwa wachezaji wanaoachwa yumo mshambuliaji huyo raia wa DR Congo.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Agha Peter alipoulizwa juu ya kuachana na mchezaji huyo alisema kila mchezaji ambaye kocha amependekeza aachwe hata kama ana mkataba na Yanga basi ataachwa.

"Ripoti ya kocha bado iko kwenye kamati ya ufundi, lakini ukweli huko hivi, mchezaji ambaye kocha amependekeza asajiliwe atasajiliwa, wa kuachwa ataachwa na wa kutolewa kwa mkopo itakuwa hivyo," alisema.

Alisema ripoti hiyo bado iko kwenye kamati ya ufundi na wakati wowote itatua kwenye kamati tendaji kwa ajili ya kuanza utekelezaji.

Suala la Molinga, Mwakalebela alisema itajulikana baadae kama anabaki au la, lakini sasa bado ni suala la ndani.