Molinga : Tulieni, tiketi ya CAF kwa Yanga bado ipo!

Muktasari:

“Mechi ngumu kwangu nilizokutana nazo hapa nchini ni zile za mwanzo zikiwamo za kirafiki ambazo zilitokana pia na mwili wangu kuwa mkubwa na mzito, kwani kipindi hicho nilikuwa nimetoka katika mapumziko ya muda mrefu kutokucheza mpira,” anasema.

JANA tulianza mfululizo wa mahojiano na straika huyu wa Yanga, David Molinga ambaye tulimfuata nyumbani kwake ana kwa ana. Alifunguka mambo kadhaa sasa endelea alipoishia utamu…!

MECHI NGUMU KWAKE

“Wapenzi wengi wa soka hapa Tanzania huwa wanafikiria mechi ngumu ni ile watani wa jadi Simba na Yanga zinapokutana, jambo ambalo si la kweli. Mechi hiyo inaweza kuwa rahisi kutokana na aina ya wachezaji wanaokutana, kila mmoja anataka kuonyesha uwezo alionao,” anasema.

“Katika mechi za watani wachezaji mnacheza kwa nafasi, hakuna mambo ya kukabana muda wote kama ilivyo katika mechi nyingine ambazo unakuta beki wa timu pinzani muda wote yupo nyuma yako kila unapokwenda anakufuata kukukaba. Katika mechi ya dabi hakuna hiyo mbinu,” anasema.

“Mechi ngumu kwangu nilizokutana nazo hapa nchini ni zile za mwanzo zikiwamo za kirafiki ambazo zilitokana pia na mwili wangu kuwa mkubwa na mzito, kwani kipindi hicho nilikuwa nimetoka katika mapumziko ya muda mrefu kutokucheza mpira,” anasema.

KILA TIMU NA UWANJA WAKE

“Nimezunguka nchi mbalimbali kucheza mpira, lakini hapa Tanzania nimevutiwa na kila timu kuwa na kiwanja chake cha nyumbani jambo ambalo katika nchi nyingine hili hakuna, unaweza kukuta timu zaidi ya tano zinatumia uwanja mmoja kama wa nyumbani,” anasema.

“Hapa Tanzania ukienda Ndanda, Mwadui, Mtibwa na nyinginezo kila moja ina uwanja wake wa nyumbani ni jambo zuri. Ila kuhusu aina ya uwanja hasa eneo la kuchezea, hilo ni jambo ambalo linatakiwa kuwekewa nguvu na kurekebishwa ili mambo yawe mazuri zaidi.

“Jambo jingine linalonivutia Tanzania kila timu kubwa kama Yanga inapokwenda, inakutana na mashabiki wengi kana kwamba wanacheza nyumbani na si ugenini kama ratiba inavyoonyesha,” anasema.

“Katika nchi nyingi kama DR Congo, timu moja inapokwenda ugenini haiwezi kukuta mashabiki wengi wanaishangilia na unaona kabisa kama mchezaji hapa tupo ugenini, lakini hilo kwa Tanzania hakuna kila Yanga tunapokwenda kucheza tunakuta mashabiki wengi.”

TIKETI YA CAF KWA YANGA

“Kuitoa Yanga katika mbio za ubingwa wa ligi hilo jambo kwangu bado, kwani kimahesabu naona tuna nafasi ya kutwaa, lakini kama wachezaji tunafahamu tuna mlima mrefu ili kulikamilisha jambo hili kwani si kazi rahisi.”

“Ila naamini kabisa Yanga tiketi yao ya michuano ya Afrika ipo kwenye Kombe la FA. Naiona Yanga ina uwezo wa kutwaa Kombe la FA na kushiriki michuano ya CAF, kutokana na muendelezo wa matokeo tuliokuwa nayo katika michuano hiyo. Kila mchezaji ana kiu ya kulifanikisha na kuipeleka Yanga michuano ya kimataifa kwa msimu ujao,” anasema.

ISHU YA BARUA YAKE

Wakati kikosi cha Yanga kilipo-kwenda kucheza mechi ya ligi dhidi ya Namungo ugenini, Molinga hakuwamo kwenye orodha ya wachezaji waliosafiri na kikosi hicho, jambo lililoibua taarifa kuwa alipewa barua ya kujieleza kwa kutokwenda huko.

Molinga anafafanua kuwa, mechi hiyo ilichezwa Jumapili, lakini siku chache nyuma alitoka kuomba ruhusa kwa kocha baada ya mkewe na watoto waliokuja siku moja kabla ya mchezo huo wa Namungo, yaani Jumamosi walikuwa wanaondoka kurejea Ufaransa.

“Kocha akanikubalia nibaki ili niweze kuisadia familia yangu kuondoka hapa nchini na kurudi nyumbani, kwani wasingeweza kuwa na amani kwa vile lugha waliyoizoea ni Kifaransa tu, hata hivyo nikashangaa baadaye kupata taarifa hizo nyingine.”

“Kwangu kuhusu suala hili kama limemalizika au bado nadhani ni mambo ya ndani zaidi ya klabu naomba niishie hapa tu kueleza, samahani,” anasema.

UFUNGAJI BORA

Molinga anasema katika mbio za ufungaji bora msimu huu, inaweza kuwa gumu kwake, kwa vile hakuanza na timu tangu mwanzo wa msimu hivyo hakushiriki yale mazoezi ya maandalizi ya msimu, ila kama msimu ujao atafanikiwa kufanya hivyo hilo kwake wala si jambo kubwa, linawezekana.

“Mshambuliaji kama Kagere (Meddie wa Simba) yupo kinara kwa misimu miwili kwa sababu kila anayemzunguka anampa sapoti kuanzia wachezaji wenzake hadi mashabiki, nami naamini kwa mwenendo huu ambao naendelea nao kutoka kwa mashabiki wa Yanga kunipa nguvu na kuniamini, naweza kuchukua tuzo hiyo msimu ujao kama nitakuwepo hapa.”

“Lakini ligi haijamalizika nakuahidi nitafunga mabao zaidi jambo ambalo naona naweza kuwashtua watu wengi. Na nafanya hivyo kwanza kutokana na biashara ambayo ipo mbele yangu. Nahitajika na timu nyingine, pia ni kwa malengo niliyojiwekea,” anasema.

TAMBI, NYAMA

“Tangu nimefika hapa nchini chakula ambacho kinanivutia kula ni tambi na nyama ambacho nimekuwa nikikipenda kabla ya kuja kuishi hapa, lakini ninao uwezo wa kukipata muda wowote ninaokihitaji,” anasema.

“Nimejikuta tu napenda kula chakula hicho. Nina imani kinanipa nguvu na hata ladha yake imekuwa ikinivutia na muda ambao nitakula huwa najisikia mwenye furaha na amani ya moyo.”

LUGHA TATIZO

“Kiukweli naweza kuzungumza Kifaransa na Kilingala kwa ufasaha, japo Kiswahili nakielewa kwa uchache jambo ambalo muda mwingine hunipa wakati mgumu kuzungumza na wachezaji wenzangu, kwani ni wachache wanaozungumza lugha hizo mbili ninazozimudu.

“Lakini kwa kuwa tunakuwa na wachezaji wote kambini, katika mazoezi na mechi muda mrefu huwa natumia Kiswahili changu kidogo kuongea na kujichanganya na wenzangu ili kuwa karibu nao na hata muda mwingine kujifundisha lugha yao,” anasema Molinga.

KUPENDEZA MUDA WOTE

“Mchezaji ni kioo cha jamii kwa maana hiyo unatakiwa kuwa mfano kwa watu wengine kwa maana hiyo binafsi napenda kuwa nadhifu muda wote na idadi ya nguo ambazo ninazo hapa nchini siwezi kuzihesabu kwani ni nyingi kiasi hata nikiondoka nitaacha nyingi kuliko ambazo nitaondoka nazo,” anasema.

“Katika idadi ya viatu nilivyonavyo hata sifahamu kwani humu ndani kwangu vipo vingi mno vinazidi 100 na nguo pamoja na viatu si kwamba naenda kununua bali kuna jamaa yangu anaitwa, Jack Collection ndio huniletea hapa nyumbani.”

MAISHA YA KAMBINI

“Maisha ya kambini na hapa nyumbani ni tofauti. Hapa huwa nafanya shughuli zangu mwenyewe nikisaidiana na mdogo wangu, ila kule kambini kila kitu tunafanyiwa na tunaishi kwa kuzingatia muda.

“Tunakula pamoja tena kwa wakati na mambo mengi huwa tunafuatiliwa na kocha au watu benchi la ufundi tofauti na nyumbani ambapo kila kitu kinakuwa chini yangu,” anasema Molinga.

WACHEZAJI ANAOWAKUBALI

“Tangu nimeanza kufuatilia au kucheza mpira kwa dunia nzima mchezaji ninayemkubali ni mshambuliaji wa Juventus, Mreno Cristiano Ronaldo amekuwa akiweka rekodi nyingi mbalimbali na kuzivunja mwenyewe hasa katika masula ya kufunga mabao, jambo ambalo linanivutia zaidi.”

“Kwa nchini navutiwa zaidi na mchezaji mwenzangu wa Yanga Mapinduzi Balama. Kwanza ni mdogo, lakini anajitambua majukumu yake uwanjani. Ambacho anafanya katika mazoezi ndicho anachoenda kukifanya katika mechi, Pia huchoki haraka. Kasi anayoanza nayo katika mechi ndio humaliza nayo.”

SAUTI ZAVUJA

“Kweli sauti zetu zilisikika kutoka katika ‘group la WhatsApp’ la wachezaji na yote hilo ilitokana na kutokuwapo na maelewano mazuri kati ya GSM na uongozi wa Yanga kutokana na pesa zilizotolewa kama motisha baada ya kuifunga Simba, ila kwangu nilichofanya ni kujitoa katika ‘group’ hilo la wachezaji wa timu kwani si salama tena,” anasema.

“Kubwa ambalo naweza kuzungumza si masuala ya kutokuwa na maelewano kati ya GSM na uongozi wa Yanga, bali ni mambo yangu ndani ya timu kama nimecheza vizuri, nimeshindwa kucheza kiwango changu kinapungua au vitu vingine vinavyonihusu mimi na si uongozi wala wadhamini,” anasema Molinga.

KIKOSI CHAKE

Molinga anasema kwa muda wote aliocheza nchini ameona wachezaji wengi wenye uwezo kutoka klabu mbalimbali, lakini kama anapewa nafasi ya kuchagua kikosi cha wachezaji 18 (wachezaji 11 wa kuanza na saba wa benchi), atafanya hivyo ila si kama wengine si wazuri.

“Kipa ningempa nafasi Faroukh Shikhalo, mabeki Juma Abdul, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’, Lamine Moro na Kelvin Yondani, kiungo nampa nafasi Jonas Mkude na Kabamba Tshishimbi wakati mawinga ni Bernard Morrison na Deo Kanda wakati mastraika ni Molinga na Meddie Kagere,” anasema.

“Katika benchi ningewapa kipa Metacha Mnata, Balama, John Bocco, Feisal Salum, Pascal Wawa, Ditram Nchimbi na Shomary Kapombe, Aiiseee nadhani hii timu haiwezi kufungwa na tutachukua ubingwa mapema kabisa,” anasema Molinga ambaye alionekana kufurahi kwa kucheka baada ya kutaja kikosi chake bora.

UJUMBE  WA CORONA

“Kwangu nipo makini na kujikinga na ugonjwa huu wa corona. Naepuka mikusanyiko kama Serikali ilivyoagiza na kutekeleza tunayoelekezwa na wataalamu wa afya.

“Pia hii naomba iwe kwa mashabiki na jamii yote. tufuate kila tunachoelekezwa na wataalam wa afya ili kuishi katika mazingira sahihi kwani ugonjwa wa covid-19 upo kweli.” Mwisho.