Moja chali Liverpool ilipigwa bao hapa tu

Wednesday May 15 2019

 

By Fadhil Athumani

SHUGHULI ndiyo ishamalizika na kama ni mwali basi kashaenda zake kwa mumewe na sasa wanafurahia maisha mapya ya ndoa. Lakini, kuchukuliwa kwa mwali huyo hakujawaacha watu salama kwani, wanaendelea kuugulia maumivu kwani, walipambana sana kutaka kumbeba ila wababe ndiyo wakafanya yao. Utafanyaje sasa inabidi kuwa mpole tu mwanangu na ujipange wakati mwingine ukisubiri apewe talaka ndipo arudishe majeshi tu.

Ndio! Manchester City ya Pep Guardiola imebeba tena ubingwa wa Ligi Kuu England baada ya kuikandamiza Brighton kwa mabao 4-1 kwenye dimba la Community. Ushindi huo ndiyo ukamaliza kelele za mashabiki wa Liverpool ya Jurgen Klopp, ambao walikuwa kwenye dimba la nyumbani, Anfield wakiichapa Wolves kwa mabao 2-0. Ubishi ukaishia hapo!

Liverpool ikamaliza msimu ikiwa nafasi ya pili, licha ya kuongoza ligi hiyo kwa tofauti ya pointi saba hadi kufikia Desemba 2018. Lakini, ni kitu gani kimewagharimu vijana wa Klopp hadi kushindwa kumnasa mwali huyo, ambaye msimu huu ilionekana mapema kabisa kwamba, watakwenda kujibebea?

Hapa Mwanaspoti linakupa sababu tano kali ambazo ndio zimelibeba jeshi la Guardiola dhidi ya Klopp.

5. KUWA NA WAFUNGAJI WENGI

Siri kubwa iliyoiwezesha City kufunga mabao 95 katika mechi 38 za ligi, ni kutokana na kuwa na mastaa wenye jicho la kupasia nyavuni ukilinganisha na Liverpool (mabao 89), ambayo kwa kiasi kikubwa yametokana na miguu ya Mohammed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane.

Man City ilikuwa na wafungaji zaidi ya 16 uwanjani, ambapo nyota nane kati yao walifunga zaidi ya mabao matano. Kwa upande wake, Liverpool, ilikuwa na wafungaji 14 huku watatu tu (Salah, Firmino na Mane), ndiyo waliofunga zaidi ya goli tano.

Ni hivi, wakati David Silva, Ilkay Gundogan, Bernardo Silva na Riyad Mahrez, walipokuwa bize kufunga mabao, wenzao wa Liverpool walikuwa na kazi ya kuwapenyezea mipira Salah, Firmino na Mane. Ndiyo maana Liverpool ililazimishwa sare saba ukilinganisha na mbili za City.

4. UONGOZI MAKINI UWANJANI

Man City kama timu inajivunia kuwa na nahodha na beki kisiki Vincent Kompany. Huyu jamaa ameibeba sana Man City na kumfanya kipa wake, Ederson kuwa salama muda wote wa dakika 90 za mchezo.

Kompany ni bonge la kiongozi uwanjani na hilo ndiyo tofauti yake na yule wa Liverpool, Jordan Henderson, ambaye zaidi ya mara moja ameonekana kupwaya katika maamuzi yake.

Wakati mwingine Virjil van Dijk, alionekana bora kimaamuzi lakini kwa Kompany alikuwa akiokoa jahazi na bao lake dhidi ya Leicester lilitoa picha kamili ya kazi yake kama kiongozi uwanjani.

Mbali na Kompany, dimbani City walikuwa na Aguero na Fernandinho ambao, kwa pamoja walilibeba jahazi la City hata wakati ambao nahodha wao hakuwapo.

3. KIKOSI CHA WASHINDI

Hebu nitajie mchezaji mmoja wa Man City, ambaye hana historia ya kushinda mataji. Hapa ndipo, ilipo karata ya ushindi ya Guardiola. Hakusajili majina tu bali alishusha majembe ya maana kwa ajili ya kufanya kazi.

Kuanzia kwa kinda wake, Aymeric Laporte, hadi mshindi wa Kombe la Dunia na Ulaya, David Silva, Guardiola alijaza wachezaji wanaojua kupambana kutafuta ushindi, hasa katika mechi muhimu kama ule wa mwisho.

Orodha ya mataji waliyochukua ni ndefu kiasi kwamba, tukianza kutaja tutamaliza ukurasa mzima. Pep, kama alivyokuwa Jose Mourinho, anaamini kuwa mchezaji hafundishwi kushinda mataji, bali anaongozwa na uzoefu.

2. KUAGA LIGI YA MABINGWA MAPEMA

Wakiwa wanapigiwa upatu kutwaa ubingwa wa Uefa msimu huu, Manchester City walijikuta wakitupwa nje na vijana wa Mauricio Pochettino, japo ilikuwa kwa mbinde kwelikweli.

Katika mechi ya raundi ya kwanza, Mkorea Son-Heung Min aliifungia Spurs bao pekee lililowapa ushindi wa 1-0, katika dimba la Tottenham Hotspurs. Wiki moja baadaye wakapiga tena shoo ya kibabe pale Etihad na kuitupa nje Man City licha ya kushinda 4-3.

Spurs wakapita kwa faida ya bao la ugenini na kuondolewa kwao kuliwapa mzuka wa kupambana kubeba taji la EPL huku wapinzani wapo wakubwa, Liverpool wakipambana na safari hadi kuichomoa Barcelona na sasa watacheza fainali dhidi ya Spurs.

1. KIKOSI KIPANA

Man City wana jeshi kubwa na lenye watu wa kazi. Kuna wachezaji 16 wamehusika kwenye mabao yake 95, hili siyo jambo la kitoto hata kidogo.

Pep alikuwa na silaha kali za maangamizi kila pembe ya uwanja. Uwanjani walikuwepo wanaume kwenye benchi hadi majeruhi nao walikuwa wakali.

Hakuwa na haja ya kutegemea wachezaji wachache kumpa kombe, kama ilivyokuwa kwa mkubwa Klopp, aliyeweka matumaini yake kwa Firmino, Mane na Salah. Hata alipomkosa Benjamin Mendy, Pep hakuwa na shaka kabisa.

Kukosekana kwa fundi Kevin de Bruyne, hakukumpa Pep presha kwa sababu kuna Bernardo Silva na David Silva. Wakati uimara wa safu ya ulinzi ya Liverpool, ikimtegemea Virgil van Dijk, Guardiola alikuwa na wanaume wanne (Kompany, Laporte, Otamendi na Stones).

Pengo la Fernandinho halikuonekana kwa sababu Gundogan na Bernardo, waliifanya kazi hiyo kwa ushirikiano mkubwa. Kutokuwa na presha, kulimsaidia bishoo wa Kihispania, Guardiola dhidi ya Mjerumani Jurgen Klopp. Lakini, siyo kesi tukutane msimu ujao.

Advertisement