Mogella: Kagere amedhihirisha ubora wa Okwi

Muktasari:

 

  • Kutokana na Meddie Kagere kushindwa kufunga dhidi ya JS Saoura staa wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella amesema amemdhihirisha Okwi kwamba asipokuwemo uwanjani ligi ya Mabingwa hawezi kufanya kitu.

Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella amesema Meddie Kagere amedhidhirisha ubora wa Emmanuel Okwi baada ya kushindwa kufunga bao dhidi ya JS Saoura, huku akigusia kitendo cha timu hiyo kutokukaa kileleni tangu kuanza msimu huu kuwa nikipimo kwa mastaa wao. 

Mogella alisema kiufundi ngumu kumfananisha Kagere na Okwi aliyedai ni mbunifu na angecheza mechi na JS Saoura wangepata matokeo.

"Ni kweli Kagere ni mpambanaji sana, ila Okwi ana kipaji cha kipekee bila kuangalia ana mabao saba kwa sasa, mbunifu na angecheza dhidi ya JS Saoura angewekewa ulinzi ambao ungewapa urahisi Bocco na Kagere kuzifumania nyavu,"alisema.

Aligeukia kitendo cha Simba kutokuonja kukaa kileleni tangu ligi ianze kwa msimu huu kwamba kuna mambo mawili faida ipo kama watafanikiwa kutetea ubingwa kutimiza msemo wa kutangulia sio kufika la ni aibu kwao.

"Itategemeana na ubora wa wachezaji kujua majukumu yao ndani ya ligi, wakishinda mechi zote kutakuwa hakuna maana kwa Yanga kuongoza ligi kwa muda mrefu halafu ubingwa wanachukua wengine la ikiwa hivyo mpaka mwisho basi kitakuwa kitendo kibaya sana kwa Simba,"alisema.

Alienda mbali na kudai kuwa wachezaji ambao wanavaa jezi nyekundu na yakijana wanapaswa kutambua kwamba wao ni kioo dhidi ya timu wanazoshiriki nazo kwenye ligi, hivyo wanapaswa kuheshimu umati wa mashabiki wanaoenda kuwaunga mkono wanapocheza.

"Sijui kama wachezaji wanajiulizaga hili swali kwamba wanapocheza baadhi ya mashabiki wanaacha shuguli zao na kwenda kuwaunga mkono, kama wanalijua hilo basi hawawezi kufanya ujinga wa kushindwa kujituma kwa bidii.

"As Vita ya Kongo iwe mfano kwa timu za Tanzania kujifunza namna walivyo na roho ya upambanaji yaani wanafanya zaidi ya kile ambacho wanaelekezwa na makocha wao, sasa huku mchezaji inakuwaje anasukumwa sukumwa,"alisema.

Mchambuzi wa soka nchini, Ally Mayay alisema Yanga kuongoza kileleni kwa muda mrefu kinawapa ujasiri wa kuendelea kupambana, tofauti na Simba ambao wanahitaji kuongeza juhudi zaidi ya kupindua meza.

 

"Kisaikolojia inakuwa inashusha ari ya kujiamini na kujituma kwa Simba kutokana na muda wote kuwaona Yanga wapo kileleni ingawa bado wana mechi nyingi ambazo dakika 90 ndiye atakuwa mwamuzi kwao"alisema.