Mo Salah bado mwaka mmoja tu Liverpool

Muktasari:

Real Madrid na Juventus zilipanga kuweka rekodi ya kumsajili Mo Salah kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, ambapo zilipeleka ofa ya Pauni 150 milioni, lakini staa huyo mwenyewe ameamua kubaki zake Anfield.

LIVERPOOL, ENGLAND.KENGELE ya hatari inagonga huko Anfield. Kubwa ni kuhusu Mohamed Salah, dirisha hili anabaki kikosini Liverpool, lakini ikifika usajili wa majira ya kiangazi mwakani, anaondoka!

Kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi, Mo Salah ameripotiwa kugomea ofa za maana kutoka kwenye timu za maana ili aendelee kubaki Liverpool baada ya kubeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Lakini supastaa huyo wa Misri ana mwaka mmoja tu wa kuendelea kubaki hapo Anfield, ikifika mwakani itakuwa vigumu kubaki.

Mo Salah ameziweka klabu kubwa huko Ulaya kwenye mkao wa kula baada ya kudai atafikiria upya hatima yake ya maisha ya baadaye katika dirisha la usajili wa majira ya kiangazi mwakani.

Real Madrid na Juventus zilipanga kuweka rekodi ya kumsajili Mo Salah kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi, ambapo zilipeleka ofa ya Pauni 150 milioni, lakini staa huyo mwenyewe ameamua kubaki zake Anfield.

Ripoti zinadai, fowadi huyo aliyefunga mabao 71 katika mechi 104 alizoitumikia timu hiyo inayonolewa na Mjerumani Jurgen Klopp, anavutiwa na mpango wa kwenda ama kujiunga na Real Madrid na kuunda kikosi cha mastaa watupu au kurudi zake Italia, kukipiga Juventus.

Lakini baada ya kuisaidia Liverpool kushinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na hivyo kuhesabika kama shujaa wa huko Anfield, Salah ameona dirisha hili si wakati mwafaka kuondoka Merseyside.

Kocha Klopp anafahamu wazi kuna vigogo wanahitaji huduma ya Mo Salah na hivyo kuwaambia mabosi wa Liverpool kujipanga na jambo hilo linaloweza kumshuhudia supastaa wao huyo akiondoka klabuni hapo. Huko Anfield hakujatulia, kumekuwa na taarifa kuwa pacha wa Mo Salah kwenye fowadi, Sadio Mane naye anasakwa na klabu nyingine. Lakini ni kama ilivyo kwa Salah katika dirisha hili, Mane naye amesema bado ataendelea kubaki Anfield kwa sasa.

Wachezaji hao wanataka kubaki Liverpool mwaka huu kujaribu kumaliza ukame wa miaka 30 wa Liverpool kushindwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England. Kama hadi kufikia mwisho wa msimu ujao na hakuna taji la Ligi Kuu England, itakuwa vigumu kuendelea kuwaona Salah na Mane huko Anfield.

Salah imefichuka mipango yake ipo thabiti kwamba kwenye dirisha lijalo la usajili wa majira ya kiangazi hiyo mwakani, amelenga kupata dili lenye mshahara mrefu na hilo linaweza kupatikana Real Madrid, ambako hivi karibuni ilimsajili Eden Hazard na wanamlipa Pauni 400,000 kwa wiki. Mwaka huu Salah anabaki Anfield kwa sababu tu ya mpango wa kupambana kwenye timu hiyo ili kubeba taji la Ligi Kuu ya England baada ya kutwaa Ligi ya Mabingwa Ulaya.