Mo Dewji awacharukia waamuzi

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Mohamed Dewji ameonekana kuchukizwa na maamuzi ya kukataliwa kwa bao la Luis Miquissone kwenye mechi ya Simba dhidi ya Mwadui jana Oktoba 31 kwa madai ya kwamba alikuwa ametoa.

Mwamuzi wa mchezo huo, Omary Mdoe kutoka Tanga alipuliza filimbi huku kibendera cha mwamuzi msaidizi, kikiwa juu mara baada ya Luis kumalizia pasi ya Clatous Chama ambayo ilizaa bao hilo ambalo lilikataliwa

Mo Dewji kupitia akaunti ya mtandao wa kijamii wa Instagram, ameposti leo Novemba Mosi kipande cha video kikionyesha wazi kuwa Luis hakuzidi kama ambavyo waamuzi wa mchezo huo walitafsiri tukio hilo ambalo limezua mjadala.

"Bado dhulma juu yetu inaendelea. Kwa mwenendo huu, mpira wetu hapa Tanzania kamwe hauwezi kusonga mbele, " ujumbe wa Mo Dewji ambaye pia ni mwekezaji ndani ya klabu hiyo, umesomeka hivyo.

Ofisa Habari wa Azam, Thabit Zakaria 'Zakazakazi' alitumia maneno ya Mo Dewji kusisitiza kuhusiana na makosa hayo ya waamuzi na kumtaka azidi kupaza sauti.

"Uko sahihi kabisa Mo. Paza sauti wewe labda utaeleweka. Mimi nilipojaribu kulalamika msimu uliopita, kuna wahuni wakasema natafuta umaarufu" ulisomeka ujumbe wa Zakaria

Licha ya bao hilo kukataliwa, Simba waliibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mwadui ambao hali yao inaonekana kuwa tete.

Hicho ni kipigo cha pili kikubwa mfululizo kwa Mwadui msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara cha kwanza walikumbana nacho, Oktoba 25 dhidi ya JKT Tanzania walichezea mabao 6-1.