Mo Dewji atajibu maswali, Barbara atapiga kazi

Wiki iliyopita Bodi ya Wakurugenzi ya Simba ilimteua mwanadada Barbara Gonzalez kuwa mtendaji mkuu wa Simba (CEO), ambapo yaliibuka maswali mengi kutoka kwa baadhi ya wadau wa michezo nchini.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo Dewji’ ndiye aliyetangaza uteuzi ya Barbara ambaye amekuwa akifanya naye kazi kwa karibu kabla hata Mo hajaingia kwenye mambo ya uwekezaji ndani ya Simba, hiyo ikiaminiwa kwamba anamfahamu vizuri juu ya utendaji kazi wake.

Maswali yaliyokuwa yanaulizwa mojawapo ni kama haya - ni lini ajira ya nafasi hiyo ilitangazwa, lini usaili ulifanyika kama ilivyokuwa awali alipoajiriwa Senzo Mazingisa, vigezo vilivyotumika kumteua yaani kwa ufupi walitaka kufahamu mchakato mzima ulivyokuwa.

Na hiyo yote ni kutokana na kwamba wengi wanafahamu ama kuzowea kwamba nafasi hiyo ni lazima ipitie michakato iliyoibua maswali akilini mwao.

Kitu pekee ambacho wadau hawakifahamu ni juu ya mamlaka ambayo inayo Bodi ya Wakurugenzi ya Simba, kwamba kwenye jambo nyeti kama hili wanaweza kuamua nini cha kufanya na kwa kipindi gani.

Hapo haijawekwa wazi, lakini inawezekana kabisa bodi ina nguvu hiyo ya kufanya uamuzi huo mzito.

Binafsi naamini Mo Dewji amesikia na anaelewa juu ya kile kilichofanywa, naamini kabisa atakuja na majibu ya maswali hayo na muongozo uliowapa nguvu kumteua mrembo huyo ambaye ni mara ya kwanza kwa soka la Tanzania kuongozwa na mwanamama hasa katika nafasi hiyo nyeti kwenye soka.

Mo Dewji afafanue vizuri kwa wadau ni kwa nini bodi imeamua kumteua na kumwamini Barbara kumpa nafasi hiyo.

Pengine haya maswali ambayo nahisi yanawasumbua baadhi yataondoka kwenye akili zao na sasa kuunga mkono juhudi za Barbara kuipeleka Simba kwenye mafanikio zaidi.

Pamoja na maswali hayo, lakini wengi wanaamini Barbara anaweza, Barbara ni mchapakazi ukiachana na kuteuliwa pengine hata kama mchakato huo ungefanyika wa kutangaza ajira na kuomba, basi hata yeye angefuata na angepita tu kama wanavyosema - kama ipo - ipo tu labda bahati ichelewe kumfikia.

Sidhani kama hili sasa linapaswa kuendelea kujadiliwa na wadau wa mchezo wa soka, Barbara anaweza na kuweza kwake sio kwa mwezi mmoja, ni lazima apewe muda na ushirikiano kutoka pande zote bodi, wanachama, mashabiki na wachezaji kwa ujumla wao ili kuhakikisha Simba inafanikiwa, naamini yote yanawezekana. Sidhani pia kama kuna sehemu imeandikwa nafasi kama hizo kubwa zinastahili kuongozwa na wanawake.

Hizo ni imani potofu hasa katika ulimwengu wa sasa, ingekuwa hivyo basi jamii ianze kufuta ule usemi wao wanaosema ‘nyumba ya mafanikio ya mwanaume basi kuna mwanamke amesimama’. Hiyo ni ishara tosha kuwa mwanaume bila mwanamke hawezi kufanya jambo likasimama ipasavyo.

Hivyo ni kiasi gani Barbara na wanawake wengine walioshika nyadhifa mbalimbali wanaweza kufanya mambo makubwa ya kimaendeleo. Wadau wasimamie tu kwenye maswali yao na si kwenye jinsia katika utendaji kazi, hakuna kazi ama nafasi ya uongozi iliyoandikwa kuwa hii ni kwa ajili ya wanaume tu. Naamini kila nafasi inashikwa na yeyote kikubwa ni kuzingatia vigezo vinavyotakiwa. Ikumbukwe kwamba hata kabla ya Senzo, bodi hiyohiyo ilimuomba Barbara awe CEO, lakini aliwagomea kwa sababu alikuwa bado anaendelea kujifunza, na sasa ametamka mwenyewe kuwa anaweza.

Mengi yamesikika lakini sidhani pia kama yana afya ndani ya Simba kwasasa, hata kama kuna jambo nyuma ya pazia lakini Wanasimba wanapaswa kuangalia maendeleo yao hivi sasa ikiwemo kukamilisha mchakato wao wa mfumo wa uendeshaji ambao mpaka sasa haujakamilika.

Mo Dewji ametamka kuwa zile Sh20 bilioni hajaziweka Simba kwasababu mchakato haujakamilika lakini amewaaminisha Wanasimba kuwa zipo na mchakato ukikamilima ataziweka, ila anaendelea kuihudumia Simba bila kujali lolote basi Wanasimba wanapaswa kuwa na subira kwa kila jambo lao ikiwemo kuwa na imani na uteuzi uliofanywa na bodi yao.

Hivyo basi Mo Dewji awatoe hofu wadau wa Simba, naamini hofu yao itatolewa kwa kujibu maswali yao juu ya mchakato uliotumika iwe kwa kuwaeleza tu kuwa utaratibu wa bodi unawaruhusu kuteua mtu yeyote mwenye vigezo kuongoza nafasi hiyo ama nyinginezo. Sidhani kama kila jambo lifanywalo linafuata Katiba, mengine ni taratibu zinazowekwa na sehenu husika. Barbara aachwe apige kazi ana kila sababu na vigezo vya kusimama kwneye nafasi hiyo nyeti, pengine hicho kiti kitamtosha kuliko viti vingine alivyowahi kuvikalia.