Mnasema Chama? Huyo Bwalya balaa

MASHABIKI wa Yanga wamekuwa na mzuka baada ya kusikia tetesi, mabosi wao wanataka kumbeba kiungo kutoka Simba, Clatous Chama, huku wale wa Msimbazi wakiwaka na kuwaambia viongozi wao ‘Huyo fundi wa mpira akiondoka mjue hatutawaelewa.”

Lakini, kumbe Yanga walikuwa na mipango yao mingine kabisa na ishu ya kumtaka Chama ilikuwa kama zuga, kwani unaambiwa mabosi hao wa Jangwani wapo katika hatua za mwisho kumalizana na kiungo mchezeshaji, Larry Bwalya kutoka Zambia.

Kiungo huyo analetwa ikiwa ni hesabu za mabosi hao kuanza kutafuta mbadala wa Haruna Niyonzima na sasa kocha wao mmoja wa zamani akawaambia utamu mzima wa kiungo huyo aliyeandika takwimu zake na kudai ni mkali zaidi kuliko hata huyo Chama wa Msimbazi.

Kocha msaidizi wa zamani wa Yanga, Noel Mwandila ndiye aliyeiambia Mwanaspoti hayo baada ya kumuuliza juu ya uwezo wa nyota huyo wa nchini kwao na kocha huyo aliyefanya kazi na George Lwandamina na baadaye Mwinyi Zahera, alisema kama kuna usajili wa maana Yanga wataufanya basi ni kumchukua Bwalya.

Mwandila alisema Bwalya kama kuna kitu anazidiwa na Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita na kiungo wa Simba, Clatous Chama basi ni uzoefu, lakini Bwalya ni hatari zaidi.

“Hapa Zambia ndiye Mchezaji Bora anajua sana kusumbua katika kiungo. Kitu pekee anachoweza kusumbuliwa na Chama basi ni uzoefu, lakini mpira anaujua hasa kama kiungo. Naona huo utakuwa ndio usajili bora kwa Yanga kama wakimpata,” alisema Mwandila.

Mzambia huyo alisema kuthibitisha ubora wake Bwalya msimu uliomalizika amefunga mabao saba na kutengeneza pasi 11 za mwisho akiwa ndiye kiungo bora akiwa na timu yake ya Power Dynamos.

“Msimu wa pili sasa anacheza kwa ubora mkubwa, anazidi kupanda. Takwimu zinaonyesha anapanda. Angalia msimu huu ameasisti pasi 11 za mabao na mbili za mwisho amezitoa katika mchezo wa mwisho wa ligi,” alisema Mwandila na kuongeza;

“Ni ngumu sana kumdhibiti akiwa uwanjani anajua kujiweka katika mazingira ya kutamani kufanya kitu katikati ya uwanja lakini ukiacha pasi za mabao pia anafunga msimu huu amefunga mabao saba.”

Alisema Yanga kama watampata Bwalya hiyo itakuwa ni kazi nzito kwa kiungo Mnyarwanda, Haruna Niyonzima kutokana na ubora wa watu hao wawili ambapo pia Mzambia huyo anaweza kucheza akitokea kati lakini pia hata pembeni.

“Nafahamu Yanga wana Haruna (Niyonzima) lakini ukiangalia watu hao wawili wanaweza kutofautiana katika madhara ya kuzalisha pasi za mwisho na hata kufunga, Haruna kama atakuwepo na Bwalya akaja hapo atakuwa amepata changamoto kubwa,” alisema na kuongeza;

“Unavyomuona Chama anavyocheza basi na Bwalya ni kama hivyo anaweza kutokea kati na hata pembeni.”

“Hapa Zambia sasa ni mchezaji muhimu katika timu ya taifa binafsi naona utakuwa ni usajili bora kwa Yanga kwa ushindani wa soka la hapo Tanzania.”

HUYU NDIYE BWALYA

Kiungo huyo amezaliwa Mei 29, 1995, ni kiungo anayetumia mguu wa kulia aliyeanza soka lake tangu akiwa kinda kabla ya kuanza kufahamika zaidi akiwa Zanaco FC kuanzia mwaka 2014 kabla ya kupita pia Nchanga Rangers na mwaka 2017 alipohamia timu yake ya sasa ya Power Dynamos.

Mbali na uwezo wa kumiliki mpira, kupiga chenga na mbio katika kuwasumbua mabeki wa timu pinzani, lakini kiungo huyo wa kimataifa wa Chipolopolo aliyoanza kuichezea tangu mwaka 2018 na mwenye umri wa miaka 25 tu kwa sasa, pia anajua kufunga, kitu ambacho kimekuwa kikimfanya akiwapelekesha washambuliaji wenye kazi zao.