Mmachinga awapa mchongo wachezaji wa Bongo

Muktasari:

  • Soka limewatajilisha wachezaji wengi duniani, wanachotakiwa wachezaji wa Tanzania kuona fursa ya kiuchumi kupitia vipaji walivyo navyo ili kubadilisha maisha yao.

Dar es Salaam. Mfungaji bora wa muda wote wa Ligi Kuu Bara, Mohamed Hussein 'Mmachinga' amesema soka kwa sasa ni dili na kuwataka wachezaji wajitoa watanufaika.

Mmachinga mshambuliaji wa zamani wa Yanga anayeshikilia rekodi ya kufunga mabao 26 msimu wa mwaka 1999 tangu wakati huo hakuna mchezaji aliyevunja rekodi hiyo alisema biashara ya soka imetanuka tofauti na zamani ambapo alidai walikuwa wanacheza kwa moyo wa uzalendo dhidi ya klabu zao.

Amekiri anaona vipaji vikubwa kwa wachezaji wa sasa kinachowasumbua wanaridhika mapema na kuporomoka viwango vyao.

"Soka lina mambo mengi na lazima mchezaji liwe sehemu yake, hapa namanisha wajitume na mazoezi ya kuwaweka fiti muda wote.

"Kubwa zaidi wajifunze kutunza miili yao kwa maana ya kuepukana na anasa ambazo hazina sababu ya kuzifanya kwa faida ya kulinda viwango vyao.

"Kuna suala la nidhamu ambalo lina upana wake kama kuzingatia muda wa kupumzika, chakula pia wajue kwamba wao ni kioo cha jamii," alisema Mmachinga