Mkutano mkuu Coastal Union nao waahirishwa

Muktasari:

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Steven Mnguto  alisema kamati ya utendaji ilikaa na kukubaliana kufanyika mkutano ambao pia ulikuwa na lengo la kuongeza wanachama wapya ambao ndio muhimili wa timu.

MKUTANO Mkuu wa Klabu ya Coastal Union uliopangwa kufanyika keshokutwa Jumapili hautafanyika kutokana na katazo la Serikali kupiga 'stop' mikusanyiko.
Hivi karibuni, Serikali ilipiga marufuku mikusanyiko ikiwa ni moja ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa corona unasambaa kwa kasi duniani.
Mkutano huo ulikuwa unakwenda sambamba na kupanga uchaguzi mkuu wa viongozi wa klabu hiyo kwani viongozi waliopo madarakani sasa muda wao wa miaka minne umemalizika.
Mwenyekiti wa klabu hiyo, Steven Mnguto  alisema kamati ya utendaji ilikaa na kukubaliana kufanyika mkutano ambao pia ulikuwa na lengo la kuongeza wanachama wapya ambao ndio muhimili wa timu.
Alisema kutokana na janga la ugonjwa huo sasa watalazimika kusubiri kwanza ambapo utapangwa mara baada ya serikali kutoa taarifa nyingine kama wataruhusu mikusanyiko baada ya siku 30 ama vinginevyo.
Katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Juni wamepanga kuongeza nafasi mbili ambazo hazikuwepo uongozi uliopita ambazo ni Afisa Masoko na Mtendaji Mkuu wa kwa lengo la kuzidi  kuborsha uendeshaji wa timu ambao utazidi kuongeza ufanisi klabuni.
Mnguto alisema uwepo wa wanachama kwenye klabu hiyo ni muhimu  sana ambapo kupitia ada ya uanachama itazidi kuongeza mapato ya timu ambayo pia itazidi  kuchangia maswala mbalimbali ya uendeshaji wa timu.
Pamoja na hayo amesema moja ya swala muhimu litakalopewa kipaumbele kwa viongozi  watakaoingia madarakani lazima wahakikishe wanafanya mchakato wa kuanza kutengeneza uwanja waliopewa na Halmashauri  ya Jiji la Tanga.