Mkude sawa, Banda mshindwe nyinyi

JONAS MKUDE

Muktasari:

  • Rais wa Simba, Evance Aveva, alikiri kwamba klabu inayomhitaji Ajib, inataka mchezaji huru na sio mwenye mkataba na ndiyo maana suala hilo lipo nje ya uwezo wao na

ABDI Banda anamaliza mkataba na Simba mwishoni mwa msimu, ila amewapa nafasi nyingine kwa wakongwe hao kama watahitaji zaidi huduma yake, lakini mabosi wa klabu hiyo wamesalimu amri kwa Jonas Mkude na Ibrahim Ajib.

Mabosi hao wa Msimbazi jana Alhamisi walikiri kuwa wanalazimika kuwaacha bure kina Mkude kwa sababu ya kushindwa kuafikiana nao na pia mipango yao ya kucheza soka la kulipwa kunakoendana na masharti ya timu zinazowataka.

Rais wa Simba, Evans Aveva amefichua kuwa, Harass El Hadood ya Misri inayomtaka Ajib ndio sababu ya kushindwa kusaini mkataba mpya wa straika huyo kwani, klabu hiyo ya Misri inataka asiwe na mkataba na klabu yoyote.

Rais wa Simba, Evance Aveva, alikiri kwamba klabu inayomhitaji Ajib, inataka mchezaji huru na sio mwenye mkataba na ndiyo maana suala hilo lipo nje ya uwezo wao na kuamua kumwacha aende bure, huku Mkude ikielezwa anataka kwenda Afrika Kusini.

“Tuliwaomba waongeze mkataba walikataa na sisi hatuwezi kuwalazimisha maamuzi yao, hivyo tupo radhi waondoke bure tu,” alisema Aveva aliyefichua uongozi wao na Baraza la Wadhamini wanaweka mambo sawa ili kuleta umoja klabuni, huku akiwaangukia wanachama 71 walioenda mahakamani wafute kesi.

“Tunawahitaji ndio maana tumeamua kuondoa tofauti ili tuwe wamoja, tukae chini tujue cha kufanya, sina wasiwasi na uwezo wa timu upo vizuri naamini tutafanya vizuri,” alisema Aveva.

BANDA HUYU HAPA

Abdi Banda naye alisema uongozi wa Simba kama unahitaji huduma zake hana tatizo mradi wakubaliane wakati wa kujadili mkataba mpya vinginevyo ataangalia utaratibu mwingine.

Banda ambaye kwa sasa yupo jijini Dar es Salaam wakati timu yake ikiwa Songea kumenyana na Majimaji, akiuguza majeraha ya mguu, ameliambia Mwanaspoti kuwa hadi sasa mawazo yake hayapo timu nyingine nchini zaidi ya Simba.

Beki huyo alisema bado hajaona tatizo la kuendelea kubaki Simba ila labda uongozi wa timu hiyo ushindwe kufikia makubaliano mapya ya kimkataba ndipo atafikiria kwenda kucheza soka la kulipwa ambako anaamini anaweza.

“Ni kweli mkataba wangu unaelekea ukingoni, hadi sasa bado sijazungumza na viongozi wangu kuhusu mkataba mpya ila Simba ndio ninayoipa kipaumbele na kama siku wakiniita kufanya mazungumzo ya mkataba mpya na tukaafikiana basi nitasaini huo mkataba.

“Lakini pia nawaangalia wao na uamuzi wao, wakishindwa kumalizana na mimi basi hapo ndipo nitaanza kuwa na mawazo mapya ya wapi niende nikacheze ila si hapa Tanzania, naelewa soka la Tanzania lilivyo na ninaielewa timu yangu na tunakwenda vizuri,” alisema.Akizungumzia juu ya majeraha yake alisema kuwa: “Leo (jana) nimekuja hospital huku kwa Dk Gilbert ila nitapumzika kwa siku 10, nashukuru naendelea vizuri na ninaweza hata kuunyanyua mguu, naamini nitakuwa fiti kabisa.”