Mkomola, Kabwili washtuliwa

Muktasari:

Chipukizi wanaopata bahati ya kuzichezea Simba na Yanga wamefundwa na wakongwe waliowahi kung'ara na klabu hizo, wameambiwa wajitambue na kujua mashabiki wanaweza wakaondoa thamani zao na kuzipandisha endapo wakifanya kile kilichowapeleka.

CHIPUKIZI wawili walioiwakilisha Tanzania katika Fainali za Afcon U17-2017, Yohana Mkomola na kipa Ramadhani Kabiwli wameumwa sikio wakitakiwa kuchangamka sasa la sivyo ndio wajue wanazika vipaji vyao ndani ya klabu ya Yanga.

Chipukizi hao walikuwa wakipata nafasi chini ya Kocha George Lwandamina, kabla ya kupotea kikosini Yanga inayonolewa na Mwinyi Zahera, jambo lililomfanya mastraika wa zamani wa kimataifa nchini, Abeid Mziba na Zamoyoni Mogella kuwashtua waamke sasa.

Mziba, aliyetamba na Yanga na Taifa Stars aliwataka wachezaji hao wajitathimini wapi walianguka kisha wasimame na kupigania vipaji vyao, kwani walipaswa wawe tegemeo ndani ya klabu yao na Taifa Stars kwa vipaji walivyonavyo.

“Angalau Kabwili katika nafasi yake kuna makipa ambao ni wazoefu wa hali ya juu, hivyo inakuwa ngumu yeye kupewa kirahisi mechi ambazo zinakuwa zinahitaji matokeo, Mkomola ajipange upya ikitokea kapata nafasi ya kucheza, asijibweteke kwa kukosa namba.”

Naye Mogella aliyekipiga Simba, Yanga na Stars alisema; “Sio kwa Kabwili na Mkomola kuna vijana wengi ndani ya kikosi hicho hata Simba wapo, nadhani kinachowaangusha ni umaarufu wanaoupata kirahisi, zamani tulikuwa tunaona mzigo sana kuitwa staa, ilitufanya tulinde viwango vyetu, wao kazi ya kunyoa viduku.”

Mogella alienda mbali kwa kumtaja Said Bahanuzi, aliyepotea kwenye ramani kirahisi.