Miyeyusho ataja kilichomkimbiza

Muktasari:

  • Bondia huyo anayetumia zaidi mkono wa kushoto (southpaw) ana rekodi ya kupigana mapambano 62 katika uzani wa light na kushinda 42, amepigwa mara 18 na kutoka sare mara 7 na sasa amepania kurejea kwa kasi zaidi ulingoni.

KAMA wewe ni miongoni mwa mashabiki wa Bondia Francis Miyeyusho au Chichi Mawe, bila shaka utakuwa ukijiuliza kipi kimemsibu bondia huyo hadi kupotea katika ramani ya ngumi.

Miyeyusho ambaye ana muda mrefu hajapigana amelitonya Mwanaspoti kwamba migogoro ndiyo ilimuweka kando kwenye ngumi.

“Tangu nilipofanyiwa figisu na kuzuiwa nisiende kucheza nje ya nchi nikiwa tayari uwanja wa ndege, nilipoteza hamasa na ngumi,” alisema Miyeyusho.

Alisema kipindi kile kilikuwa kigumu kwani alitumia nguvu kubwa kujiandaa na pambano hilo la nje, lakini viongozi waliokuwa kwenye ngumi hawakujali hilo.

“Nilitulia nikisubiri migogoro ipite, bahati nzuri Serikali imeliona hilo na sasa ngumi zimeanza kutulia na hivi karibuni, Waziri Mwakyembe (Harrison) alituita mabondia na kutuweka sawa kuhusu muelekeo wa ngumi.

“Hamasa hiyo imenirejesha upya katika ndondi na mashabiki wasubiri mambo mazuri ulingoni, hapa sasa ni kazi kazi, najifua kweli kweli kurudi katika ubora wangu,” alisema Miyeyusho na kuongeza migogoro siku zote inarudisha nyuma maendeleo ya mchezo kwa sababu kila kinachofanyika hata kama ni kizuri lazima litokee kundi litakalolipinga.

Bondia huyo anayetumia zaidi mkono wa kushoto (southpaw) ana rekodi ya kupigana mapambano 62 katika uzani wa light na kushinda 42, amepigwa mara 18 na kutoka sare mara 7 na sasa amepania kurejea kwa kasi zaidi ulingoni.