Miujiza ya Ligi Kuu Tanzania mechi 10 zaondoka makocha tisa

Tuesday December 3 2019

Miujiza- Ligi Kuu Tanzania- mechi 10 -zaondoka makocha tisa-rekodi-mashindano-chalenji-

 

By Olipa Assa

Dar es Salaam. Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), inasimama kupisha mashindano ya Chalenji yatakayoanza Desemba 7, 2019, Uganda huku ikiwa imeacha rekodi mbalimbali za kusisimua.

Hadi ligi hiyo inaingia katika mapumziko Yanga imecheza mechi chache zaidi nane, huku nyingine zikiwa zimecheza 10 ya juu zaidi ni 13.

Mwanaspoti online linakukusanyia rekodi zilizofanywa kwenye mechi zilizochezwa kabla ya ligi kusimama.

Makocha tisa wametimuliwa

Hakuna ubishi kwamba ligi mwaka huu imeshuhudi timuatimua ya makocha kuanzia siku ya kwanza hadi siku ya mwisho ya mapumziko.

Makocha hao wametimuliwa kwa sababu mbalimbali wengine ni kutokana na nguvu za mashabiki au viongozi kukosa Imani nao.

Advertisement

BILO-ALLIANCE

Athuman Bilali 'Bilo' ndiye alikuwa wa kwanza kuachana na Alliance, alitoa sababu kwamba alikuwa anaingiliwa majukumu yake na uongozi wa timu hiyo, nafasi yake ilizibwa na Habibu Kondo.

MINZIRO-SINGIDA UNITED

Aliyekuwa kocha wa Singida United, Fred Felix Minziro aliamua kuachana na timu hiyo kwa madai hapewi heshima inayostahiki, hivyo nafasi yake ikachukuliwa na Ramadhan Nsanzurwimo.

ZAHERA-YANGA

Yanga iliamua kumfungashia virago kocha wao Mwinyi Zahera kwa kile kilichodaiwa hawakuridhishwa na matokeo na wakaamua kumkabidhi mikoba mwalimu Charles Mkwasa.

MAYANJA-KMC

Matokeo hovyo ya mechi mfululizo iliyopata KMC chini ya Jackson Mayanja ndio sababu ya kumtimua ndani ya kikosi hicho na sasa inafundishwa na mwalimu Hamadi Ali.

AUSSEMS-SIMBA

Simba imemfungushia virago kocha wao Patrick Aussems licha ya timu hiyo kuongoza ligi, sababu ikitajwa kuwa ni kushindwa kusimamia nidhamu ya wachezaji, msaidizi wake Denisi Kitambi amepewa majukumu ya kusimamia timu ndani ya wiki moja.

MWAMBUSI-MBEYA CITY

Nongwa za mashabiki kutomhitaji kocha Juma Mwambusi kulimfanya kocha huyo kuandika barua ya kutohitaji kuendelea na majukumu ndani ya timu hiyo, kikosi hicho kinanolewa na Mohamed Kijuso.

MALALE-NDANDA FC

Ndanda FC haikuhitaji kuendelea na kocha Malale Hamisi badala yake imemchukua Amri Said kwa muda.

AMRI SAIDI-BIASHARA

Biashara iliamua kuachana na kocha Amri Said kutokana na timu hiyo kushindwa kupata matokeo mazuri, timu hiyo kwa sasa ipo chini ya mwalimu Omary Madenge.

NDAYIRAGIJE-AZAM FC

Azam FC haikumtimua kocha Etienne Ndayiragije, iliamua kumwachia baada ya kupata dili kwenye kikosi cha Taifa Stars, hivyo timu hiyo kwa sasa ipo chini ya kocha Arastica Cioaba.

NYOTA ZAO ZIMENG'AA

Kuna wachezaji ambao nyota zao zimengaa kwenye mechi walizocheza kama Meddie Kagere wa Simba inayeongoza kwa mabao 8, Paul Nonga (Lipuli mabao 7), Deruesh Seif (Lipuli mabao 6) na Miraji Athuman (Simba mabao 6).

Ditram Nchimbi wa Polisi Tanzania yeye hana idadi kubwa ya mabao, anamiliki matatu aliyofunga hat-trick dhidi ya Yanga hilo ndilo lilimfanya ang'ae na kuandika rekodi yake mpaka sasa.

TIMU ZILIZOCHEMKA

Singida United ipo katika wakati mgumu zaidi kwani katika mechi 13 iliyocheza imepata ushindi mechi moja, imetoka sare minne na imefungwa nane, hivyo imejikusanyia pointi saba.

Timu nyingine ambazo zimefanya hovyo ni Mbeya City ina alama nane katika mechi 12 walizocheza, Ndanda FC ina pointi nane imecheza mechi 13 na KMC ina alama tisa imecheza mechi 11.

WAMEIBUKIA HUKU

Pius Buswita ameibukia Polisi Tanzania baada ya kukaa nje alipotemwa na Yanga, hivyo ataanza kuitumikia timu hiyo kwa mkataba wa miezi sita.

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

Advertisement