Minziro: Tulieni mambo mazuri bado yanakuja

HUKO Geita Gold FC mambo ni moto unaambiwa, kwani baada ya kuanza kwa kishindo Ligi Daraja la Kwanza, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Fred Felix ‘Minziro’ amewataka mashabiki kutulia akisisitiza kuwa mambo mazuri yanakuja.

Timu hiyo ya mjini Geita kwa takribani misimu minne imekuwa ikihaha kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu, ambapo msimu huu imeonekana kuja kivingine ikibeba matumaini kwa mashabiki.

Ikumbukwe kuwa timu hiyo iliposhiriki Daraja la Kwanza kwa mara ya kwanza ilikumbana na kibano cha kushushwa daraja kwa kashfa ya upangaji wa matokeo katika mechi ya mwisho ikiwa na JKT Oljoro, JKT Kanembwa na Polisi Tabora.

Pia, katika misimu miwili mfululizo Geita Gold imekuwa ikiishia hatua ya mchujo ikitolewa na timu za Ligi Kuu katika dakika za mwisho na msimu huu imesisitiza kuwa lazima kieleweke.

Katika mchezo wa juzi ambao ulikuwa wa kwanza, Geita Gold ikiwa uwanja wake wa nyumbani iliiadhibu Singida United kwa mabao 2-0 na kutua nafasi ya pili ikiwa na pointi tatu ikizidiwa bao moja na vinara wa kundi B, Fountain Gate.

Minziro alisema kuanza vyema kwa ligi hiyo kunawapa nguvu kuendelea kufanya vizuri na kufikia malengo yao ya kucheza Ligi Kuu.