Mingange afichua siri Azam

Muktasari:

  • Tutapambana mpaka dakika ya mwisho kwani hakuna anayejua matokeo ya mechi zilizosalia bila kucheza na ndio maana pamoja na kushinda mfululizo tumetoka sare na Mbao,” alisema.

KOCHA wa Azam FC, Meja Mstaafu, Abdul Mingange amefichua siri ya kutofungwa tangu timu hiyo aipokee kutoka mikononi mwa Hans Pluijm kuwa alitengeneza usawa kwa wachezaji ili kila mmoja ajisikie sehemu ya klabu.

Mingange alisema usawa uliopo kwenye timu hiyo umetengeneza uelewano baina yao na wachezaji na viongozi wa klabu, hivyo wanafanya majukumu yao kwa urahisi.

“Kama timu inakuwa na uelewano ni silaha kubwa, kwani mnakuwa na nguvu ya kuweka nia ya kuitimiza kwa pamoja, hilo ndilo linalotendeka ndani ya Azam ndio maana tumeshinda mechi mfululizo na sare dhidi ya Mbao. Kitu ninachoweza kuwaambia mashabiki wa soka, bado hatujajitoa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Bara.

Tutapambana mpaka dakika ya mwisho kwani hakuna anayejua matokeo ya mechi zilizosalia bila kucheza na ndio maana pamoja na kushinda mfululizo tumetoka sare na Mbao,” alisema.

Mingange alisema kikosi chake kwa sasa kina ari ya kutaka kufanya kitu cha kihistoria katika mechi nane zilizobakia kumaliza msimu huu na hata michuano ya FA kuhakikisha wanachukua ubingwa.