Michael Wambura: Karia hana ujanja, awe mpole tu!

Saturday December 8 2018

 

By MWANAHIBA RICHARD

KWENYE soka kuna mambo mengi yanafanywa ambayo baadhi ni kwa ajili ya maendeleo ya soka na mengine yanarudisha nyuma maendeleo hayo.
Kuna migogoro iliyozoeleka kwa klabu kongwe nchini Simba na Yanga ambayo miaka ya nyuma ilikuwa kama ndiyo njia ya mafanikio kwao, bila migogoro klabu hizo zilikuwa haziwezi kwenda. Hiyo ilikuwa ni kasumba yao tu japo sasa imepungua na huenda ikamalizika kabisa kama watakubali kubalidilika kulingana na teknolojia inavyokuwa.
Lakini hivi sasa tunaanza kuona migogoro hiyo ikihamia kwenye Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambalo ndilo mlezi wa soka, kumekuwepo na mivutano na manung'uniko kwa wadau mbalimbali juu ya shirikisho hilo linavyoendeshwa sasa.
Hadi sasa ni zaidi ya wajumbe saba ambao wamefungiwa kifungo cha maisha na Kamati ya Maadili ya TFF jambo ambalo halijawahi kutokea kwenye uongozi wa shirikisho hilo miaka ya nyuma ukilinganisha na sasa chini ya Rais Wallace Karia ambaye ana zaidi ya mwaka mmoja pekee tangu achaguliwe.
Mapema mwaka huu, Michael Wambura ambaye ni Makamu wa Rais wa TFF alifungiwa kutojihusisha na soka katika maisha yake yote kwa tuhuma za kupokea na kuchukuwa fedha  za TFF za malipo ambayo si halali kinyume na sheria za shirikisho hilo ambapo baadaye alifungua shauri Mahakama Kuu Tanzania.
Mahakama hiyo baada ya kusikiliza pande zote mbili, Wambura na TFF ilitoa hukumu ya kumrejesha kwenye majukumu yake kama Makamu wa Rais kwa kile kilichoelezwa kwamba hukumu iliyotolewa na Kamati ya TFF haikuzingatia kanuni wala sheria.
Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti yaliyofanyika jijini Dar es Salaam, Wambura alielezea mambo mbalimbali yaliyojitokeza kwa kipindi chote hicho kama ifuatavyo;

KAMATI ZA TFF
Wambura anaeleza kwamba kwa mujibu wa Katiba ya TFF na FIFA kamati zote zinapaswa kuteuliwa ama kuundwa na mkutano mkuu, lakini TFF hakuna kamati iliyoteuliwa na mkutano mkuu zaidi ya wajumbe wa kamati ya Utendaji ambao walichaguliwa na wanachama.
"Katiba ya TFF imesiginwa sana tu, kamati zinazoundwa si kwa mujibu wa Katiba ambayo inaelekeza Kamati kuundwa na mkutano mkuu. Kamati za kisheria zinapaswa kuwa huru na sio kuingiliwa majukumu yake.
"Hilo lipo wazi, wale wanaofahamu vizuri wanaelewa nini kinaendelea ndani ya TFF kuhusiana na kamati hizo, mkutano mkuu ukiteua Kamati inasaidia kuondoa ukiritimba, pia kila Kamati inapaswa Mwenyekiti na Makamu wake wote wawe wanasheria wenye uwezo mkubwa kisheria na kimahakama," alisema

MAHAKAMA YA KIRAIA
Wadau mbalimbali wanajiuliza kwanini Wambura anapenda kukimbilia kupeleka mambo ya mpira kwenye mahakama za kiraia wakati kuna mahakama ya michezo CAS, yeye anafafanua juu ya hilo.
"Kama watu wanasoma ama wamesoma Katiba ya TFF wataelewa kwanini naenda mahakama za kiraia kutafuta haki yangu ya msingi. Katiba ya TFF imesajili chini ya sheria za nchi na sio Mahakama ya Usuluhishi ya kimichezo ya kimataifa (CAS).
"CAS ni chombo tu cha usuluhishi na wao wakishindwa wanakwambia uende mahakama za kiraia kutafuta haki yako.
"Huwa naenda mahakamani kwasababu mimi ni raia wa Tanzania na Katiba ya TFF imesajiliwa chini ya sheria ya nchi, hivyo sehemu pekee ya kupata haki ni huko, nilipopeleka malalamiko yangu mahakama iliangalia mfumo mzima wa hukumu yangu ilivyoendeshwa.
"Waliangalia kama ilifuata sheria ya nchi, je walitenda haki, uzuri kila shauri linapotoitishwa kusikilizwa hata TFF walifika, hivyo hakuna sehemu yoyote niliyokosea na yule atakayenielewa ni yule tu anayeielewa vyema Katiba ya TFF na sheria za nchi," alisema
"Kwenye Katiba ya TFF Ibara ya 74 (4) inasema Kamati ya Maadili ndiyo yenye maamuzi ya mwisho na kifungu cha 48 kinaelezea mwenendo wa mashauri ambapo Cas itasikiliza rufaa kutokana na maamuzi ya chombo na sheria ya nchi inasema hakuna mtu wa kupinga maamuzi ya mwisho ya Mahakama Kuu ya Tanzania hilo lipo wazi.
"Sasa hapo ningeenda huko ningesikilizwaje maana wangekosa uwezo wa kunisikiliza kwani hawatanitambua kwasababu hukumu ilitolewa na kamati ambayo ni chombo cha mwisho cha TFF ndiyo maana hata hao CAS huruhusu kwenda mahakama za kiraia mtu asiporidhishwa na hukumu yake,"

KATIBA YA TFF
Kutokana na kusiginwa kwa Katiba ya TFF, Wambura alishauri kufanya marekebisho ya Katiba hiyo kama FIFA walivyoagiza miaka ya nyuma ambapo hadi sasa hawajaifanyia marekebisho na kuendelea kuwa na makosa mengi ya kisheria.
"Katiba ya TFF inaweza kuwavuruga wadau wake, FIFA waliagiza tufanye marekebisho ya Katiba ila hakuna kilichofanyika hadi sasa, Katiba haina Baraza la Usuluhishi ambalo linatambulika na FIFA na walitueleza kuwa lazima liwepo ambalo hata mambo mengine yangekuwa yanaishia huko bila kufika makahamani.
"Sasa hapo nani ana makosa, mimi nipeleke malalamiko yangu CAS ambako hawatutambui, napeleka huko kama nani, maana hata nikiulizwa kama nimepitia Baraza la Usuluhishi nitashindwa kuwajibu, hata hilo suala la kutopeleka mambo ya michezo mahakamani lipo kwa mdomo tu, yote haya yalipaswa kuwekwa kwenye Katiba ya TFF," alisema Wambura na kusisitiza ili mambo yakae sawa TFF ni lazima wakubali kurekebisha katiba yao na kufuata maagizo ya FIFA.

ANAPENDA HAKI
Wambura, wengi wanafahamu kwamba ni mtu wa kukimbilia mahakamani lakini yeye anafafanua; "Mtu asiyejua haki yake hawezi kwenda mahakamani, ila mimi najua haki yangu na sehemu ya kupatikana ndio maana naenda mahakamani na ninashinda.
"Ni kweli nimekwenda sana mahakamani, tangu miaka na miaka kwani nimekuwa nikikutana na vigingi vingi hata kwenye uchaguzi wakati huo TFF inaitwa FAT, Simba ni kwa vile wanaoongoza ni watu wale wale wanaozunguka hivyo kila sehemu unakutana nao,"

FEDHA ZA FIFA
"Nchi za Ulaya zinapewa mgawo wao wa kila mwaka kwasababu ni waadilifu kwenye fedha na hawana migogoro ya ajabu ajabu, lakini nchi 19 za Afrika ikiwemo Tanzania hazijapewa mgawo wao, ukiachana na matumizi mabaya ya fedha lakini migogoro inayoendelea kwenye mashirikisho yao pia yanachangia kwa kiasi kikubwa kukosekana kwa fedha hizo, msipokuwa sawa ndani ya shirikisho hawatoi pesa.
"Ndio maana namshauri Rais Wallace Karia ajitahidi kuondoa mipasuko ndani ya shirikisho lake kwani inaharibu mambo mengi sana ya maendeleo ya soka letu," alisema Wambura.

MAMBO MATATU YA KARIA
Kwa mtazamo wa Wambura amemshauri Karia kufanya mambo matatu endapo ataona moyo wake hauna amani kufanyakazi pamoja na Makamu wake ambayo ni
"Moja, atekeleze maamuzi ya mahakama, vinginevyo atasababisha matatizo makubwa ndani ya taasisi hiyo.
"Pili, akiona kufanyakazi na mimi haiwezekani ama hatakuwa huru aende kwenye mkutano mkuu akayaseme hayo hao ndiyo watakaoamua maana ndio waamuzi wa mwisho.
"Tatu, kama hawezi vyote viwili hapo juu basi aitishe mkutano mkuu na kuwaomba waridhie kufanya uchaguzi mkuu maana yeye hataweza kujiuzulu, ili viongozi wachaguliwe upya kwa ajili ya faida ya soka na Taifa kwa ujumla," alisema Wambura ambaye yupo tayari kufanyakazi na Karia

KWANI KUNA BIFU HAPA
"Kama ana tatizo na mimi basi hajaliweka wazi ila sikumbuki kama nimewahi kutofautiana naye, hakuna shida baina yetu ndiyo maana nasema nipo tayari kufanyakazi na bosi wangu, nilichaguliwa na wanachama hivyo sina sababu ya kujiuzulu wanachama ndiyo watakaoniondoa," alisema
"Kabla sijaenda mahakamani nakumbuka  Aprili 3, tuliwaandikia barua TFF kuomba kukutana nao ili kujadili juu ya hili lakini hadi tunakwenda kufungua shauri mahakamani Mei 29, hawakujibu chochote, ndiyo maana shauri liliendelea kusikilizwa hadi lilipotolewa hukumu Novemba 30," alisema
"Hakuna sehemu yoyote inayosema karani wa mahakama ndiye anayepaswa kupeleka nyaraka za hukumu TFF ama sehemu nyingine, nilipeleka mwenyewe kwasababu mimi ndiye mwathirika na inaruhusiwa, hii ni kunisaidia mimi kuwa na uhakika kama nyaraka zimepokelewa ili wakishindwa kuyafanyia kazi yale yaliyoamuriwa iwe rahisi kwamba kurudi mahakamani kuomba mwongozo mwingine.
"Ingawa nina uhakika hata wao wenyewe TFF wameenda mahakamani kuchukuwa hukumu hiyo, ninachosubiri ni Rais Karia kuitikia wito wa mahakama ikiwemo barua niliyomwandikia ya kuomba kukutana naye ili kujadili mambo mbalimbali ya maendeleo ya TFF.
"Makamu wa Rais hapaswi kukaa ofisini muda wowote lakini kila kitu kitajulikana baada ya barua hiyo niliyomwandikia Karia jinsi atakavyoipokea na kuijibu," alisema Wambura.

Advertisement