Miaka minane ya Leseni za klabu, Tanzania inahaha

Club Licensing (leseni za klabu) changamoto nyingine katika soka la Tanzania, licha ya Fifa na Caf kutoa mwongozo katika kusimamia suala hilo lakini nchini bado ni changamoto kwa klabu nyingi.
Club Licensing ni nini?
Huu ni mfumo ambao ulianzishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) kwa ajili ya maendeleo ya soka ukilenga maeneo mbalimbali muhimu.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF) lilifuata mkondo huo kwa kutaka kila nchi mwanachama kuhakikisha inafuata utaratibu wa leseni za klabu ambao unaweka misingi bora kwenye soka.
Mfumo wa Club Licensing huko hivi
Mpango huo ulianisha mambo mbalimbali ambayo Fifa na Caf iliona yakitekelezwa yatasaidia kwa kiasi kikubwa kunyanyua soka.
Ulitaka klabu kuwa na programu za vijana, viwanja vyenye viwango vya mechi na mazoezi, sekretarieti, hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka na mambo mengine kadha wa kadha.
Tanzania hali ikoje?
Mfumo huo uliopitishwa na kamati ya utendaji ya CAF, Januari 19, 2012 na kuanza kutumika Machi Mosi, mwaka huo ulitaka klabu kuwa na uwanja wake wa mechi na wa mazoezi.
Pia ulizingatia dhana ya utawala bora kwa viongozi wa soka pamoja na uendeshaji wa soka la vijana.
Kwa Tanzania, pamoja na kwamba kuna ugumu kukamilisha mfumo huo moja kwa moja, lakini aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Shirikisho la Soka (TFF), Angetile Osiah anasema inawezekana kutekeleza kimoja baada ya kingine kwa kukitungia kanuni ambazo zitaongoza soka.
Anasema kuna mambo ambayo yanawezekana kufanyika sasa na mengine yatakuwa yakifanyika taratibu.
“Kama tukifanikisha kuingia kwa dhati katika mpango huo utasaidia mambo mbalimbali ikiwamo soka la vijana kwani huko ndipo ilipo mizizi ya soka.
“Hapo zitaangaliwa zaidi academy (vituo vya kukuza soka)na watoto ambao huangaliwa zaidi ni wale wenye umri chini ya miaka 13, na kwa kawaida umri huo hawaangalii zaidi jinsia kwani kinachofanyika wote huwekwa timu moja na kuwachanganya kwa sababu hapo hufundishwa ile misingi ya soka,” anasema Osiah.
Baada ya CAF kupitisha mfumo huo Januari, 2012, miezi michache baadaye iliingiza sheria ya club licensing kutokana na maagizo ya CAF, lengo lilikuwa kila klabu mwanachama wa TFF ijiendeshe katika utaratibu huo.
Misingi ya Club Licensing iko hivi
Club Licensing imeyapa vipaumbele mambo mbalimbali kwa lengo la kuendeleza soka na kuwa na utawala bora katika misingi ya mpira wa miguu kote duniani kwa klabu kuzingatia, miongoni mwa mambo hayo ni programu za vijana.
CAF ilitaka kila klabu kuwa na programu za vijana ambazo zitahusisha timu za vijana ambazo hizo ndizo msingi wa soka kote duniani.
Katika programu za vijana wameanisha klabu kuwa na kocha mkuu wa kikosi cha kwanza, kocha mkuu wa programu ya maendeleo kwa vijana na kocha wa vijana ambao hao kwa nyakati tofauti wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa manufaa sio tu ya klabu kuwa na timu imara ya vijana, hata nchi itakuwa na kikosi kipana cha vijana.
Uwanja uliothibitishwa
Katika kipengele hiki, CAF imezitaka klabu kuwa na uwanja wa mechi na wa mazoezi ambao aidha utakuwa ukimilikiwa na klabu au klabu iwe imeingia makubaliano na wamiliki wa uwanja huo.
Katika uwanja wa mechi inataka uwe na vyumba kwa ajili ya waamuzi, taa, majukwaa, sehemu ya matibabu na kupima doping (dawa za kuongeza nguvu), alama za kuchezea (mfano kona - flag) na eneo ambalo watu wenye ulemavu watakaa.
Haikuishia hapo inaelezwa uwanja uwe na nyasi asili na kama ni nyasi bandia, basi ziwe kwa mujibu wa viwango vya Fifa na CAF. Uwanja uwe na hoteli pia kama mojawapo wa vitu vya ziada vilivyoainishwa katika klabu mfumo huo.
Sekretarieti ya klabu
Hili ni jambo jingine ambalo limeainishwa katika mfumo huo ukiachana na viongozi wa kuchaguliwa.
Katika kipengele hiki pia klabu inapaswa kuajiri sekretarieti.
Mlolongo huo utaanzia katika ajira ya katibu mkuu wa klabu, mhasibu, msemaji na mweka hazina ambao watakuwa wakiwalipa mishahara na watahudumu kama waajiriwa wa klabu.
Anwani ya klabu
Kwa Tanzania sio tu kwenye soka, kwenye baadhi ya michezo kuna vyama na klabu ambazo ofisi zao ziko mfukoni, jambo ambalo CAF na Fifa wameliona na kuliwekea mkazo wa kulikomesha katika kupitia mfumo huu.
Klabu inapaswa kuwa na ofisi, anwani na iwe na muundo wa mawasiliano unaojumuisha simu, fax, internet na e-mail ili kuwapa urahisi wahusika kupatikana pale wanapohitajika.
Aidha mfumo huu umetaka klabu kuwa na meneja au mtendaji mkuu, ofisa wa fedha, daktari na mchua misuli. Pia iwe na idara au kitengo cha ulinzi.
Hesabu zilizokaguliwa kwa mwaka
Katika mambo ambayo yanaviingiza vyama au klabu katika migogoro ni fedha, hivyo kwenye mfumo huu unataka klabu iwe na hesabu zilizokaguliwa za mwaka.
Kama haitoshi, iainishe mali za klabu na zile ambazo klabu inazo lakini sio mali zake.
Pia, iainishe mali ambazo inazo lakini haziingizii faida mfano Yanga inalo jengo lakini hawajapangisha, hivyo haliwaingizii faida na ile ambayo inazo na zinaiingizia faida kama jengo la Simba lililopo pale Msimbazi ambalo limepangishwa.
Lakini pia vitu ambavyo vinaitwisha klabu gharama kama vile magari na mambo mengine muhimu.
Endapo klabu ina hisa itaje thamani ya hisa, kodi, mapato na faida pamoja na hasara katika mali za klabu na namna inavyohamisha wachezaji au pesa. Swali je? Tanzania imefanikisha hayo kwa kiasi gani?.
Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Iddi Kipingu anasema sio yote yanaweza kufanyika nchini kwa wakati mmoja lakini vingewekwa vipaumbele kipi kianze na kipi kisubiri.
Anasema yale ambayo yapo ndani ya uwezo wa klabu za Tanzania yapewe kipaumbele na yale yaliyo nje ya uwezo yafanyike polepole kwa kutungiwa sheria.
“Ni heri kufanya yale ambayo yanawezekana kuliko kutofanya kabisa, siku Fifa au CAF wakija kubaini itakuwa ni jambo jingine,” anasema.
Ofisa mtendaji mkuu wa Bodi ya Ligi, Almas Kasongo anasema moja ya vipaumbele vyake ni utekelezaji wa mfumo wa leseni kwa klabu.“Huu ndio mpango mzima kama tunahitaji kutoka hapa tulipo na kupiga hatua katika soka,” anasema.
Anasema watahakikisha mpango huo unaendana na uhalisia katika soka la Tanzania kabla ya 2021.
“Kuna vitu ambavyo tutaanza navyo, hasa suala la viwanja, mahesabu na sekretarieti,” anasema.
Anasema mfumo huo unataka uwanja wa mechi uwe wa kiwango bora wenye nyasi, uwe na ulinzi na uzio ambao utatenganisha mashabiki na eneo la kuchezea, uwe na vyumba vya maofisa wa mchezo na vya kubadilishia nguo, chumba cha madaktari, lakini kuna viwanja havina vitu hivyo.
“Kuna viwanja vingine ukienda hata ubao wa kuonyeshea magoli haupo, katika hilo hatutalifumbia macho,” anasema.
Anasema jambo lingine ambalo linawezekana kuanza nalo ni muundo wa utawala wa klabu.
“Hili tutaweka mkazo, bahati nzuri club licensing imeeleza klabu zinahitaji kuwa na viongozi wa aina gani na je klabu kweli zinakidhi hilo?
“Katika hesabu, club licensing inasema klabu ambayo itakuwa ikidaiwa aidha na wachezaji wake au watumishi wake, haipaswi kupewa leseni ya kushiriki ligi, tutaliangalia hilo katika kila msimu.
“Namna gani pia zinaripoti taarifa za fedha, bajeti zao na namna wanavyopata idhini ni sawa, hivyo vinawezekana kuanza navyo sasa na vingine tutakuwa tukifanya polepole kwa miaka miwili au mitatu.
2021 zitakazoshindwa kutoshiriki Ligi
Kasongo anasema hadi kufikia 2021, klabu ambayo itashindwa kuenenda katika mambo aliyoyaainisha itakuwa imejipunguza yenyewe kushiriki ligi, hasa zile za Ligi Kuu.
“Kwa kuwa tunaelekea kupunguza timu kutoka 20 mpaka 16 kwenye Ligi Kuu ambazo zitashindwa kukidhi matakwa ya club licensing niliyoyaainisha itabidi zitupishe.
“Hili halitakuwa na mzaha katika uongozi wangu, hatupaswi kurudi nyuma kwa masilahi ya soka la Tanzania,” anasisitiza Kasongo.
Anasema pamoja na kwamba sio jambo jepesi kwa nchi kama Tanzania klabu kufuata muundo huo, lakini kama kuna nia inawezekana na kupita njia ambazo wenye mpira wao duniani wanataka lakini pia itakuwa na manufaa kwa nchi.
Bodi itaweza?
Hata hivyo, Osiah kwa upande wake anasema mfumo wa soka la Tanzania kwa sasa msimamizi ni TFF kwani hata Bodi ya Ligi bado inafanya majukumu yake kwa asilimia kubwa kutokana na maelekezo ya TFF.
Anasema sio jambo jepesi la kufanya kwa haraka haraka, “lakini tukiamua linaweza kuanzia kwenye timu za Ligi Kuu, wakati likishuka taratibu kwenye timu za ligi za chini.
“Mfano tunaweza kusema timu zote za Ligi Kuu ndio zinatakiwa kuanza na baadaye unapeleka kwa timu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na mwisho Ligi Daraja la Pili (SDL).”
Tanzania ilifeli wapi mwanzo?
Ni miaka minane sasa imepita tangu kuanzisha kwa mfumo huo ambao Osiah anasema: “Wakati unaanzishwa (akiwa katibu mkuu TFF), tulianza na viwanja, tulitaka timu zote mwanzoni mwa msimu ziseme viwanja vyao vya nyumbani ni vipi.”
Anasema walianza na viwanja ili iwe rahisi kwenye upatikanaji wa wahusika ili watu wa ‘dopping’ ikitokea wamekuja ghafla, wakihitaji timu fulani inajulikana ilipo, lakini pia kukaguliwa ubora wa viwanja hivyo na ikawezekana.
Athari yake ni kufungiwa
Moja ya athari kubwa kwa timu kushindwa kukidhi matakwa ya mfumo huo ni kufungiwa kushiriki ligi au mashindano husika endapo CAF na Fifa itabaini uwepo wa ujanjaujanja katika hilo.
Osiah anasema faida ni nyingi zaidi katika mfumo huo kwani timu itajiendesha kwa misingi sahihi, lakini pia itasaidia klabu kujiendesha kisasa na hata ukuaji wa soka katika nchi inayopitia mkondo huo utakuwa mkubwa.
Vigogo wa klabu wafunguka
Wakati swali likiwa ni vipi klabu za Tanzania kushindwa kufuata mkondo huo tangu ulipoasisiwa miaka minane iliyopita, klabu mbalimbali zimeanika sababu na kuweka mikakati.
Katibu mkuu wa Tanzania Prisons, Ajab Adam Kifukwe alisema wamepata elimu ya kutosha kuhusu jambo hilo japo hapo awali waliliona kama kitu kigumu kukitekeleza, lakini hivi sasa kila kitu kimekaa sawa kwa upande wao.
“Kila timu inatakiwa kuwa na viwanja vya mazoezi pamoja na ule wa kuchezea, anwani tunayo na siku si nyingi tutajenga uwanja wa mazoezi kwani Magereza ina maeneo mengi hivyo tuko katika mchakato huo,” alisema.
Mwenyekiti wa Mbeya City, Emmanuel Kimbe alisema ili kupita katika matakwa ya mfumo huo klabu yao imeanza ‘kutoka usingizini’.
“Uwanja wa ligi tunao wa Sokoine, tunafikiria kujenga uwanja wetu wa mazoezi, lakini pia ofisi tunayo na muundo wa uongozi uko vizuri, mengine tutaendelea kuyaboresha polepole,” alisema.
Mmoja wa wakurugenzi wa Bodi ya Simba, Salim Abdallah (Try Again) alisema tayari wana uwanja wao wa mazoezi ambao una viwango vyote na uwanja wa mechi wanatumia ule wa Mkapa ambao pia sio wa kuuliza kuhusiana na viwango.
“Klabu yetu tunajiendesha kisasa, huenda kutakuwa na mambo madogomadogo ambayo yatapandishwa kuongezwa, lakini katika suala la club licensing tuko vizuri,” alisema.