Mh! Arsenal kubaniwa tena kwa Mario Gotze

Muktasari:

Mkataba wa sasa wa staa huyo huko Dortmund itafika tamati 2020, lakini mabosi wa timu hiyo wanataka kumpa dili jipya ili kumtibulia Emery, ambaye alikuwa akiamini angemnasa staa huyo na kumleta kwenye Ligi Kuu England.

LONDON, ENGLAND.KOCHA wa Arsenal, Unai Emery anaelekea kukwama kwenye mpango wake wa kumnasa Mario Gotze baada ya Borussia Dortmund kudai ipo kwenye mazungumzo ya kumwongezea mkataba supastaa huyo wa Kiargentina.

Emery alikuwa akipiga hesabu za kumnasa Gotze, kwa sababu anafahamu wazi atampata kwa dili la chini kidogo, huku msimu uliomalizika hivi karibuni huko kwenye Bundesliga alionyesha kuwa fiti na hakusumbuliwa na majeruhi.

Mkataba wa sasa wa staa huyo huko Dortmund itafika tamati 2020, lakini mabosi wa timu hiyo wanataka kumpa dili jipya ili kumtibulia Emery, ambaye alikuwa akiamini angemnasa staa huyo na kumleta kwenye Ligi Kuu England.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Dortmund, Michael Zorc alisema mpango wa timu hiyo ni kumbakiza Gotze kwenye kikosi chao, alisema: “Tumesikia tetesi nyingi za kutoka England kwa miaka mingi. Lakini, kama kawaida yetu, siku zote tumekuwa hatuna wasiwasi.

“Gotze hajatufuata kuomba kuhama. Na kwa sasa tumekuwa kwenye mazungumzo mazuri na baba na wakala wake. Mwanzo wa msimu ujao, tutaketi na kuzungumza kuhusu mkataba mpya.”

Arsenal imekuwa ikihusishwa na mpango wa kumsajili Gotze tangu mwaka 2011 kipindi hicho alipoibukia kwenye soka akiwa kinda mdogo na kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger alisema wakati ule: “Gotze ni mchezeshaji, ni mmoja kati ya wachezaji wazuri kwa asisti Ujerumani na pia ni mchezaji hatari.”

Arsenal ilikwama kumsajili Gotze, akaenda zake Bayern Munich kwa muda mchache kabla ya kurudi zake tena Dortmund.