Mguto na mipango yake TPLB

Muktasari:

  • Uchaguzi huo pia ulichagua nafasi mbili za wajumbe kutoka klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na klabu za Ligi Daraja la Pili (SDL).

Tanga.WIKIENDI iliyopita Bodi ya Ligi (PTLB) ilifanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi za viongozi waliojiuzulu akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti, Clement Sanga na wajumbe wawili.

Uchaguzi huo ulifanyika jijini Tanga na Steven Mguto alichaguliwa kuwa mwenyekiti kwa kura 16 kati ya 18 huku wajumbe wawili kutoka klabu ya Yanga na African Lyon wao hawakufika kabisa ili watimize idadi ya wapiga kura 20 kutoka klabu za Ligi Kuu.

Mguto alikuwa mgombea pekee katika nafasi hiyo baada ya wapinzani wawili, Emmanuel Kimbe na James Bwire kupigwa chini kwa kile kilichoelezwa kukosa sifa za kugombea kwani wagombea hao walidaiwa hawakuwa wenyeviti wa klabu zao bali ni wakurugenzi na kikanuni hawaruhusiwi kugombea nafasi hiyo.

Uchaguzi huo pia ulichagua nafasi mbili za wajumbe kutoka klabu za Ligi Daraja la Kwanza (FDL) na klabu za Ligi Daraja la Pili (SDL).

Mwanaspoti ambalo lilikuwepo kwenye uchaguzi huo uliokwenda sambamba na Mkutano Mkuu wa TPLB lilifanya mahojiano maalumu na Mguto ambaye atakaa madarakani kwa kipindi cha miaka minne na kueleza mambo mbalimbali baada ya kushinda uchaguzi.

AMETIMIZA NDOTO

“Kuchaguliwa kwangu kuna maana kubwa sana, kwanza nimetimiza ndoto yangu ambayo nilikuwa nikiiota siku zote ipo siku nitaongoza taasisi niliyopo sasa.

“Muda mrefu nilikuwa na ndoto ya kuhakikisha natoa mchango wangu katika mpira nikiwa kama kiongozi sasa nimefikia mafanikio.

“Kuchaguliwa kwangu wananchi, wadau wa soka wanasubiri kuona nini nitakifanya katika soka hasa Bodi ya Ligi na dhamira yangu ni ipi,” alisema.

VIPAUMBELE

“Mpira wetu unakua kila kukicha lakini kuna vitu vinakwamisha na nimepanga kuvishughulikia ili kuondokana kabisa na changamoto hiyo.

“Moja wapo ni kuhakikisha naondoa tatizo la upanguaji wa ratiba inayovurugika mara kwa mara kwa sababu imekuwa ikilalamikiwa na wadau wa soka nchi.

“Pia kuna changamoto ya uchezeshwaji mbovu wa Ligi Daraja la Kwanza na la Pili ambako nimeshuhudia mwenyewe nikiwa na timu yangu ya Coastal Union, hivyo nakemea vitu ambavyo nimeviona.

“Kuna ukandamizwaji hasa kwa timu za Polisi na Jeshi, nazungumza kwa sababu ni wanachama wa Bodi ya Ligi wakifanya vitu visivyofaa lazima waambiwe,” alisema.

UDHAMINI TPL

Ligi Kuu msimu huu haina udhamini na klabu zimekuwa zikijiendesha katika mazingira magumu na Mguto ameelezea changamoto hiyo;

“Sio sahihi ligi yetu kukosa mdhamini, kuna mambo yanachangia kukosekana kwake moja wapo ni pamoja na kupewa thamani kubwa ambayo haistahili.

“Japo hilo siliamini sana, ligi yetu ni nzuri na kubwa lakini klabu zake hazijielewi kwa sababu hazifahamu zinataka nini katika mpira, pia kushuka kwa uchumi ambao umezikumba kampuni nyingi kumechangia kwa kiasi fulani.”

MAPATO

Klabu kwa kushirikiana na bodi hiyo zilikubaliana timu ambayo ni mwenyeji wa mchezo kuchukua mapato yote ya mechi husika jambo ambalo sasa linaonekana kuzigharamu baadhi ya timu hasa zenye uwezo mdogo kifedha pale zinaposafiri kumfuata mwenyeji.

Mguto anafafanua hilo; “Hakuna ubaya wowote kwa upande wangu naona ni sawa kwa sababu unatoa changamoto kwa timu mwenyeji kujitangaza kwa mashabiki ili wajitokeze kwa wingi uwanjani na kupata kipato kikubwa kutokana na jinsi mashabiki watakavyoingia kushuhudia mechi husika.”

Anasema kwa upande wa timu yake ya Coastal Union wanataabika na hilo kutokana na kupoteza mashabiki wengi baada ya kuporomoka kwa viwango na kujikuta inaingia kwenye changamoto ya kushuka daraja na kupanda.

“Mechi zinazotunufaisha ni Simba na Yanga ambazo ndizo zina mashabiki wengi kila mikoa kutokana na kufanya kwao vizuri hivyo ni jukumu letu kuhakikisha tunawarudisha mashabiki.”

Je, baada ya mipango hiyo, Mguto anafikiria nini kuhusu TFF inapokosea? Vipi kuhusu udhamini wa ligi za chini? Ungana naye kesho kutwa Alhamisi ili kujua hilo na mengine mengi.