Mgosi afichua siri nzito ya Luis Simba

Muktasari:

Luis ameonekana kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo, huku wakitarajia kuona makubwa zaidi kwake kama alivyoahidi bado hajafikia kiwango anachokitaka.

NAHODHA wa zamani wa Simba ambaye ni miongoni mwa wachezaji waliojenga heshima Msimbazi, Musa Hassan ‘Mgosi’ amesema winga Luis Miquissone anaitendea haki jezi yake.

Katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti, Mgosi ambaye alikuwa anavaa jezi namba 11 ambayo anaitumia mchezaji huyo raia wa Msumbiji amesema tangu atundike daruga mwaka 2016 hakuna mchezaji aliyeitumia vyema namba hiyo kama anavyofanya Luis.

Anasema jambo hilo pekee limefanya ajione amerejea upya uwanjani kutokana na kiwango cha nyota ambaye amefunga magoli matatu hadi sasa tangu asajiliwe wakati wa dirisha dogo la usajili msimu huu. Awali tangu Mgosi aondoke jezi hiyo imewahi kuvaliwa na Laudit Mavugo, Marcel Kaheza na Wilker da Silva.

Luis ameonekana kuwapa raha mashabiki wa timu hiyo, huku wakitarajia kuona makubwa zaidi kwake kama alivyoahidi bado hajafikia kiwango anachokitaka.

“Hakuna mchezaji duniani kote ambaye akistaafu atafurahia jezi yake ikivaliwa na mtu mwenye kiwango duni, wakati yeye alikuwa kwenye uwezo mkubwa.

“Ndio maana nasema wachezaji wa zamani waulize watakwambia maana kuna wakati wachezaji wakicheza kiwango cha chini, wanatamani waingie wawaonyeshe ufundi ila nyakati zinakuwa zimewatupa mkono, akili zinataka miili haipo tayari,” anasema Mgosi ambaye kwa sasa ni kocha wa Simba Queens inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake.

Alizitaja sifa za mchezaji huyo kwamba ndani yake ana uzalendo licha ya kuipa thamani kazi yake pia amekuwa akijitoa mpaka tone la mwisho timu ipate matokeo.

“Tangu niivue jezi yangu, Luis anaitendea haki, kutokana na jinsi anavyojituma kuhakikisha timu inapata matokeo, kila ninapomuona napata faraja ya kipekee.”

Anaongeza “Ni miongoni mwa wachezaji wa kigeni wanaoleta chachu kwenye soka la Tanzania anajua nini anakitaka soka, mpira ukiuheshimu utakuheshimu.

“Kikubwa ajiepushe na vitu vitakavyoweza kumuondoa kwenye mstari, asione anajua ama amefika anapaswa kuendelea kujifunza na kutaka kufika mbali zaidi,”anasema Mgosi ambaye licha ya kuzaliwa familia ya soka yeye ndoto yake ilikuwa ufundi magari.

WAZAWA VS WAGENI

“Zamani akija mchezaji wa kigeni alikuwa anajua kweli, mfano walikuwepo ndani ya kikosi cha Simba kuna Mnaigeria alikuwa anaitwa Orji Obinna, Mganda George Owino, Mkenya Moses Odhiambo hawa jamaa hawakuwa wa mchezo

“Yanga walikuwepo Keneth Asamoah, John Baraza, Mike Baraza na Mbuyu Twite, baadaye wakawa wanaletwa wachezaji wakawaida tu kabla ya miaka hii miwili kuleta wenye uwezo tena,”anasema.

Anasema wazawa wanaridhika wakipewa 50 milioni za usajili basi wanaisahau kesho yao. “Kutojitambua kwa wazawa linatokana na kutothamini kazi, wakipata umarufu basi watu wanakoma mtaani, soka linahitaji heshima, kutamani kucheza vizuri zaidi ya leo, sasa wengi wanatembea na historia ya nikifanya vizuri jana na leo hana jambo,”anasema.

DAU LA SIMBA MIL.5

Anasema alipewa 5 milioni aliposajiliwa Simba zilikuwa nyingi alikwenda kuwekeza kwenye aridhi na mambo mengine.

“Kwanza nilipewa 3 milioni baadaye 2 milioni nikaja nikamaliziwa baadaye, sikutaka kuchezea pesa hiyo muda wote nilikuwa nawaza maisha yangu ya baadaye,”anasema.

“Yanga iliniboreshea maisha yangu kwa Simba, nikipewa mkataba naenda nao Simba basi wao wananipa zaidi na mkataba unakuwa mkubwa,”anasema mchezaji huyo ambaye alijiunga na Simba ikiwa na fundi Ulimboka Mwakingwe ambaye umri wake hawakupishana sana.

“Yaani jamaa alikuwa balaa, mpaka leo sijaona winga kama yule kwenye Ligi Kuu Bara, kasi, akili, kupambana, vilinifanya nijitume zaidi,” anasema.

SAMATTA VS MSUVA

Anasema yeye ndiye alitangulia kwenda kucheza soka la kulipwa Congo katika klabu ya Motema Pembe kisha akafuata Mbwana Mbwana Samatta kwenda TP Mazembe ambako hakuanza moja kwa moja kucheza.

“Nilijiunga na Motema Pembe nikiwa na kiwango cha juu hivyo haikunisumbua kuanza kikosi cha kwanza, bahati mbaya mdogo wangu Samatta hakuanza moja kwa moja, jambo ambalo lilikuwa likimuumiza.

“Akawa ananiambia kaka sipendi kukaa benchi, nikawa namwambia vumilia jitume kila kitu kitakwenda sawa, akaanza kucheza na mpaka akapata mafanikio ya hali ya juu,” anasema.

“Huwa naongea naye sana, nataniana naye kuwa umevuka zaidi ya kile ulichokitamani, naombea aendelea kufanya maajabu zaidi ya pale alipo.

“Binafsi natamani thamani yake iwe kubwa ndani ya Aston Villa ili aendelee kuonekana na timu nyingine kwani anaitangaza Tanzania na wachezaji wengine wameonekane,” anasema.

MSUVA ALIJIITA MGOSI

Anasema Usimba na Yanga ndio ulimfanya Simon Msuva anayekipiga Morocco kuacha kutumia jina la a.k.a yake ya Mgosi.

Anasema kabla ya Msuva hajasaini Yanga alikuwa anakaa naye kwake kipindi fulani, hivyo timu za mtaani alizokuwa anazichezea walimtambua kwa jina la Mgosi.

“Nilichukua jukumu la kukaa naye kwa sababu niliona kipaji chake unajua namna mashabiki wa Yanga walivyo wasingeweza kujiita Mgosi lakini bado tuna mawasiliano ya karibu sana,” anasema.

MECHI BORA KWAKE

Anasema wakati ametoka kusajiliwa Simba alikaa kwa muda mchache benchi, na kuna siku alipewa nafasi katika michuano ya Tusker Cup iliyochezwa Mwanza ambapo nusu fainali wakicheza na Sports Villa ya Uganda akafunga bao la kuwapeleka fainali.

“Fainali tulicheza na Yanga, ambapo tuliwafunga mabao 2-1 tukawa mabingwa bao moja nilifunga mimi,” anasema.

AMEWAFUNGA YANGA

MARA NYINGI

Anasema msimu wa 2004/06 kila alipokuwa akikutana na Yanga alikuwa anafunga bao hata kama Simba itapoteza mchezo.

“Nimewafunga Yanga mara nyingi hata kama Simba ikifungwa mabao 2-1 mimi nilikuwa nafunga, nilikuwa na mzuka na mechi hizo, ndio maana walikuwa wanapambana kunisajili,”anasema mchezaji huyo aliyewafunga mabao matano Yanga kwa nyakati tofauti.

Anasema hakumbuki mwaka lakini Yanga iliposhinda bao 1-0 aliumia sana huku yeye akipaisha mpira akiwa yeye na kipa.

Alimpiga chenga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ , Mbuyu Twite na kipa alikuwa Mserbia kufika golini mashabiki wa Simba wanaanza kushangilia akapaisha bahati mbaya.

“Nililia kama mtoto, niliishiwa nguvu, mashabiki wakaanza kuniambia nimechukua pesa, kama sio viongozi wa Simba na familia yangu nilikuwa nimeamua kuacha soka.

“Nikawaambia viongozi naacha soka kutokana na jinsi nikivyokuwa najisikia vibaya,nilitoka kwenye ari ya kufanya kazi kabisa, nashukuru Mungu walikuwa na hekima wakanijenga nikasimama upya,” anasema.

SIMBA YA SASA NA ZAMANI

“Vijana hawaonyeshi uzalendo pesa mbele, ndio maana wanakuwa kwenye viwango vikubwa msimu mmoja unaofuata wanapotea,”anasema.

“Mfano kuna Luis Miquissone, Claytous Chama, Meddie Kagere na wengine miongoni mwa wageni wanaofanya vizuri sana Simba,”anasema.

Katika kikosi cha Yanga ni wachezaji wawili tu ndio anaona bora nyakati zote kwake ambao ni Papy Tshishimbi na Haruna Niyonzima.

Alipoulizwa unakionaje kiwango cha Benard Morrison? Alijibu kuwa “Kuna wachezaji wengi wa aina yake waling’ara mechi chache wakapotea ila tofauti na heshima ya Niyonzima na Tshishimbi ambao muda wote wapo kwenye viwango vilevile jua sio wamchezo mchezo.”

Unajua kama Mgosi aliwahi kukimbia jeshini? Anasema nini kuhusu Ndemla na Kichuya? Kama asingekuwa mchezaji wa soka unadhani angekuwa anafanya nani?

Usikose kesho Jumamosi