Mgeta: Mbongo aliyesaka Ligi Kuu Ujerumani kwa jasho

Muktasari:

  • Mgeta anasema baada ya kukumbana na changamoto hiyo na umri nao kusogea ndipo alipoamua kujikita rasmi kwenye ligi za madaraja ya chini ambazo na zenyewe zimekuwa na changamoto mbalimbali.

BEKI wa Kitanzania, Emily Mgeta ambaye alitua Ujerumani 2015 akitokea Polisi Moro lengo lake lilikuwa ni kucheza Ligi Kuu nchini humo ambayo ‘Bundesliga’.

Mambo yalienda kombo kwa Mgeta wa VFB Eppingen licha ya uwepo wa juhudi za msimamizi wake, Arnifred Lemle ambaye ndiye aliyefanikisha kutua kwake nchini humo baada ya kuvutiwa na kiwango chake.

Mgeta anasema wakati anawasiliana na Lemle alikuwa akimweleza kuwa ni siku nyingi amekuwa na ndoto za kucheza Bundesliga na alivutia na namna nilivyokuwa na shauku hiyo, alimweleza kuwa anaweza kuanzia chini kisha akatimiza ndoto zake.

“Baada ya kufika Ujerumani nilifanya majaribio katika Timu ya Neckarsulmer SU inayoshiriki Ligi Daraja la Tano (verbandsliga), niliweza kufuzu majaribio yangu na ikawa timu yangu ya kwanza nchini humo.

“Mkataba wangu ulipomalizika nilijiunga na Sportfreunde Lauffen ambayo nayo pia inashiriki Ligi Daraja la Tano, niligundua kuwa kuna ugumu wa kucheza ligi za daraja ya juu kutokana na kutoka kwangu kwenye taifa ambalo viwango vyake vya soka vipo chini,” anasema.

Mgeta anasema baada ya kukumbana na changamoto hiyo na umri nao kusogea ndipo alipoamua kujikita rasmi kwenye ligi za madaraja ya chini ambazo na zenyewe zimekuwa na changamoto mbalimbali.

Akiwa Ujerumani Mgeta anasema amekutana na changamoto nyingi ambazo zimemfanya ajifunze vitu mbalimbali ambavyo anaamini vitamsaidia kwenye maisha yake.

“Nimejifunza uwekezaji na uendeshaji wa soka kwa weledi zaidi, pia huku kuna kutanua akili jinsi ya kujipanga kimaisha baada”

“Nimejidhatiti vya kutosha kupambana katika hali yoyote ili nifanikiwe, hivyo changamoto hizi nakabiliana nazo vyema ili nitimize malengo yangu,” anasema.

Mgeta ambaye ni Mzaliwa wa wilaya ya Ukerewe mkoani Mwanza anasema alianza kucheza soka akiwa kidato cha tatu ambapo alipata nafasi ya kucheza mashindano ya vijana ambayo ni maarufu kama Copa Coca-Cola, 2009.

“Nikapita katika akademi ya Tanzania Street Children Academy (Tsca) ya mkoani Mwanza kuanzia 2009-2010, nikaenda akademi ya Tinsela ya wilayani Magu mkoani Mwanza.

“Kisha nikarejea tena TSCA. Baada ya siku chache kurudi TSCA tulisafiri mpaka Arusha kwenda kushiriki michuano ya Rollingstone Cup.

“Katika michuano ile tulitolewa robo fainali na kurudi nyumbani Mwanza. Baada ya kurejea nilipigiwa simu na kiongozi wa Tinsela Bw. Geoffrey Tinsela, akinitaarifu kuwa natakiwa kwenda jijini Dar es Salaam katika mchujo wa Timu ya Taifa ya vijana U-20 ‘Ngorongoro Heroes’.

“Nawashukuru sana makocha Kim Poulsen na Adolph Rishard ambao waliniamini na kunichagua katika timu ile na kujumuishwa katika kikosi kilichoshiriki Cosafa ya U-20 nchini Botswana ambapo tulitolewa hatua ya robo fainali.

“Baada ya kutoka Botswana katika michuano ya Cosafa, nikiwa najiandaa kurudi Mwanza nilipigiwa simu na Mutani Yangwe Mkurugenzi wa TSCA akinijulisha kuwa nisiondoke na badala yake niende nikaonane na kiongozi wa Simba B Patrick Rweyemamu, ili kujiunga na Simba B.

“Nilijiunga na Simba B, mwaka 2012. Mafanikio niliyoyapata ni pamoja na kuchukua vikombe vya Kinesi Cup na lile la Bank ABC,” anasema.

“Nawashauri vijana wapatapo nafasi za kutoka wazitumie, wasijiulize mara mbilimbili watoke kwa wingi wasiogope changamoto kwani huu ndio wakati wao, ukizingatia vijana wengi wanafanya vizuri sana,” anasema.