Messi amtaja kocha mpya Barcelona

Monday July 27 2020
messi pic

HAKUNA uhakika kama Kocha wa Barcelona, Quique Setien ataendelea kumnoa supastaa Lionel Messi. Ndio, mambo bado ni magumu na yanaweza kutibuka zaidi kama Barca itashindwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Lakini, tayari mwenye Barcelona yake, Messi amemtaja kocha mpya ambaye angependa aende kuwanoa msimu ujao. Huyu ni Marcelo Bielsa, ambaye ameipandisha Leeds United kucheza Ligi Kuu England msimu ujao.

Bielsa, ambaye ni raia wa Argentina kwa sasa ndio habari ya mjini baada ya kuweka rekodi hiyo ambayo makocha wenzake waliotangulia walisota kwa miaka 16 bila mafanikio.

Kupigwa kikumbo kwenye mbio za ubingwa wa La Liga, kumemfanya Setien kuwa kwenye presha kubwa licha ya hivi karibuni kudai mzozo wake na Messi umekwisha.

Mkataba wa Bielsa na Leeds United umemalizika jana na mpaka sasa mchawi huyo wa soka mwenye miaka 64, hajasaini mkataba mpya.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwenye korido za Nou Camp ni kwamba, Messi ambaye amekuwa na sauti kubwa inapokuja suala la kuchagua kocha wa kuja kuinoa ama kusajili mchezaji, amewaambia mabosi zake kuwa Bielsa anastahili kupewa mikoba ya Setien.

Advertisement

Messi, 33, amewaambia mabosi zake wafanye haraka kuzungumza na Bielsa kwa kuwa, mkataba wake na Leeds United umamalizika hivyo yuko huru.

Alisema kwa hali ya mambo ilivyo, Barca inaweza kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na hilo linaweza kutokea kwenye mchezo dhidi ya Napoli kama Setien atabaki klabuni hapo.

Setien aliyechukua mikoba ya Ernesto Valverde aliyefutwa kazi Januari, mwaka huu, kwa matokeo mabovu, ameingia kwenye mgogoro na baadhi ya mastaa wake huku Messi akikosoa mbinu zake za ufundishaji hadharani.

Mbali na Bielsa, pia kuna makocha wengine ambao wanatajwa kwenda kuinoa Barca akiwemo nguli wao wa zamani, Patrick Kluivert na kiungo wa zamani wa miamba hiyo Xavi Hernandez, ambaye kwa sasa ni kocha wa Al-Sadd ya Qatar.

Advertisement