Messi, Ronaldo wazua vijembe

BARCELONA, HISPANIA. BARCELONA wamewacheka wenzao wa Juventus baada ya kuwachapa 2-0 juzi Jumatano - walipowaambia: “Tumefurahi mmemwona mwanasoka bora zaidi uwanjani kwenu.”

Mashabiki hao walikuwa na maana ya Lionel Messi, ambaye aliongoza vyema Barcelona kupata ushindi huo kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati wa mchezo uliofanyika Turin, Italia.

Hata hivyo, mashabiki wa Juventus hawakuwa na furaha kwa sababu supastaa wao, Cristiano Ronaldo hakucheza mechi hiyo kutokana na kupimwa kwa mara ya tatu na kukutwa na virusi vya corona.

Katika mchezo huo, Alvaro Morata alifunga hat-trick -lakini mabao yake yote hayo yalikataliwa na VAR.

Na Messi aliwafanya vibaya Juventus, aliasisti bao la Ousmane Dembele, kabla ya yeye mwenyewe kufunga kwa penalti katika dakika za majeruhi kuifanya Barcelona kuondoka uwanjani na pointi zote tatu.

Hata hivyo si suala la ushindi tu, bali Barcelona walitumia ukurasa wao wa Twitter kuwasakama Juventus maneno ambayo ni kijembe cha moja kwa moja kwa Ronaldo.

Barca ilitwiti hivi: “Tumefurahi mmemwona mwanasoka bora uwanjani kwenu”

Juventus walijibu kwa kuwaambia wanasubiri mechi ya marudio Desemba 8.

Mabingwa hao wa Serie A walijibu: “Bila shaka mtakuwa mmetazama kamusi ya uongo. Tutawaletea mwenyewe huko Camp Nou.”

Mastaa hao wawili, rekodi zao za mabao katika michuano yote, Messi amefunga mara 637 na Ronaldo 641.

Ronaldo ametisha pia kwenye soka la kimataifa, amefunga mara 101 katika mechi 167, wakati Messi amefunga mabao 71 katika mechi 140.